Jun 11, 2021 07:58 UTC
  • Ufaransa yasitisha Operesheni ya Barkhane eneo la Sahel, Afrika

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kuwa nchi hiyo karibuni hivi itasitisha Operesheni ya Barkhane ya eti kupambana na magenge ya kigaidi katika eneo la Sahel la Afrika.

Macron alitangaza hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, Ufaransa itaanza kutekeleza usitishaji huo kwa kupunguza idadi ya wanajeshi wake walioko katika eneo hilo la Magharibi mwa Afrika, na kwamba itajumuishwa idadi ndogo ya askari wake kwenye kikosi cha kimataifa.

Amedai kuwa serikali ya Paris haiwezi kufanya kazi na kushirikiana na serikali (za nchi za eneo la Sahel) ambazo zinaendelea kufanya mazungumzo na magenge ya kigaidi.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema Macron ametoa tangazo hilo siku moja kabla ya kuanza mkutano wa viongozi wa kundi la G7 unaofanyika kati ya leo na Jumapili nchini Uingereza, na vile vile kongamano la muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO litakalofanyika Juni 14 mjini Brussels; kwa shabaha ya kuzishinikiza nchi za Magharibi ziisaidie Ufaransa kubeba mzigo huo wa eti kupambana na ugaidi katika nchi za eneo la Sahel, zinazojumuisha Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

Askari wa Ufaransa nchini Mali katika Operesheni ya Barkhane

Licha ya Ufaransa kutuma askari 5,100 katika eneo la Sahel barani Afrika katika operesheni hiyo iliyopewa jina la Barkhane kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, lakini eneo hilo lingali linasumbuliwa na mashambulizi na ukatili mkubwa wa makundi ya kigaidi yenye mfungamano na makundi ya Daesh (ISIS) na al-Qaida.

Ni vizuri kuashiria hapa kuwa, kampuni nyingi za madini na nishati za Ufaransa zinafanya kazi katika maeneo hayo ya Afrika. Vikosi ajinabi katika eneo la Sahel vimekuwa vikikosolewa kwa kuua raia wasio na hatia katika mashambulio yao hususan ya anga, kwa kisizingizio cha kupambana na ugaidi.      

 

Tags