Jun 11, 2021 12:23 UTC
  • Russia yaanza mazoezi ya kijeshi eneo ambako Marekani pia inapanga mazoezi ya kivita

Jeshi la Majini la Russia limeanza mazoezi makubwa ya kijeshi katika eneo la kati mwa Bahari ya Pasifiki punde baada ya Marekani kusema itafanya mazoezi makubwa zaidi ya kivita katika eneo hilo hilo katika msimu wa joto mwaka huu.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa taarifa ikisema: “Kwa mujibu wa mpango wa mafunzo ya ya kijeshi ya majeshi yetu katika Kamandi ya Pasifkii mwaka 2021, manoari za vikosi vya pamoja zinafanya mazoezi katika eneo hilo la mbali baharini.”

Manoari ya Ukanda wa Pasifiki za Jeshi la Majini la Russia zimeenda masafa ya kilomita 4000 hadi kufika eneo la mazoezi, imesema taarifa hiyo. Mazoezi hayo yanajumuisha meli za kivita, nyambizi na ndege za kivita.

Mazoezi hayo ya kijeshi ya Russia yanafanyika baada ya Jeshi la Marekani kutangaza mwezi jana kuwa makumi ya maelfu ya wanajeshi wake watafanya mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi katika miongo ya hivi karibuni ikiwa ni katika kujitayarishwa kwa ajili ya makabiliano tarajaiwa baina yake na China na Russia.

Rais Putin wa Russia

Hivi karibuni Rais Vladimir Putin wa Russia aliapa kuwa atayalinda kwa nguvu zote maslahi ya taifa hilo huku akilaani vikali kile alichokitaja kuwa ni chuki dhidi ya Russia au "Russophobia”.

Matamshi hayo ya Putin yametolewa huku mivutano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani ikiongezeka sana hivi sasa.

Ijapokuwa mivutano baina ya Umoja wa Ulaya na Russia iliongezeka mwaka 2014, hata hivyo mivutano hiyo imweshadidi sana tangu alipoingia madarakani rais mpya huko Marekani, Joe Biden.

Tags