Jun 12, 2021 13:10 UTC
  • Maelfu waandamana kulaani 'Islamophobia' nchini Canada

Maelfu ya watu wamefanya maandamano makubwa nchini Canada kulaani vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, sambamba na kuonesha mshikamano wao na familia moja ya Kiislamu iliyouawa hivi karibuni katika mji wa London jimboni Ontario nchini humo.

Katika maandamano hayo, maelfu walitembelea kwa zaidi ya kilomita saba, kutoka eneo walikouawa Waislamu wanne raia wa Canada waliokuwa na asili ya Pakistan, hadi karibu na eneo alikokamatwa Nathaniel Veltman, katili aliyetekeleza unyama huo mjini London.

Jumapili iliyopita, kijana huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu (20) aliua watu wanne wa familia moja na kujeruhi vibaya mwingine, baada ya kuwagonga kwa makusudi na lori lake katika mkoa wa Ontario. Ushahidi unaonesha kuwa hatua hiyo ya kigaidi ilipangwa tangu hapo awali na halikuwa tukio la sadfa.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji katika maandamano ya jana yalikuwa na jumbe zinazosema "Chuki haina nafasi hapa" na "Mapenzi badala ya chuki."

Abdullah al-Jarad, mwanachuo mwenye umri wa miaka 19 aliyeshiriki maandamano hayo amesema, "kilele cha maandamano haya si idadi kubwa ya watu waliojitokeza, bali ni mseto wa watu wa dini, madhehebu na imani tofauti waliojitokeza." 

Maafisa usalama katika eneo walikouawa kikatili watu wanne wa familia ya Kiislamu London, Canada

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau aliyataja mauaji hayo kama shambulio la kigaidi, na kuahidi kupambana na magenge yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini humo.

Takwimu zilizotolewa na Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 kumefanyika hujuma na mashambulizi 300 dhidi ya Waislamu nchini humo na kwamba, zaidi ya mashambulizi 30 yaliambatana na ukatili mkubwa. 

Tags