Jun 13, 2021 02:50 UTC
  • Waandishi habari wa Marekani wataka kuakisiwa jinai za Israel katika vyombo vya habari vya nchi hiyo

Zaidi ya Waandishi wa habari 500 wa Marekani wamesaini barua ya pamoja wakitaka kuakisiwa na kutangazwa habari zinazohusiana na dhulma na siasa za kibaguzi za Israel huko Palestina.

Barua ya waandishi hao wa habari wa Marekani imetoa wito kwa vyombo vya habari nchini humo kukomeshwa mtindo wa kuficha uvamizi wa Israel na ukandamizaji wa kimfumo wa utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Barua hiyo iliyosainiwa na waandishi 514 wa habari wa Marekani wakiwemo waandishi wa vyombo vikubwa vya habari kama Washington Post, Wall Street Journal, na Los Angeles Times imesisitiza kuwa, kuweka wazi haki na kweli na kuwawajibisha wenye nguvu na madaraka ni miongoni mwa misingi muhimu ya uandishi wa habari, lakini inasikitisha kuwa vyombo vya habari vya Marekani vimetupilia mbali msingi huo katika habari zinazohusiana na mzozo wa Israel na Wapalestina.

Imesema: "Tumekuwa tukitoa riwaya inayoficha kiini cha kadhia ya Palestina yaani uvamizi wa kijeshi wa Israel na mfumo wake wa ubaguzi wa Apartheid."

Zaidi ya Wapalestina 250 wameuawa katika mashambulizi ya Israel, Ukanda wa Gaza

Barua ya waandishi hao imesisitiza udharura wa kukomeshwa mwenendo huo mbaya ambao imesema unaendelea kwa kipindi cha miongo kadhaa sasa.

Waandishi hao zaidi ya 500 wa Wamarekani wamesema, ushahidi wa ukandamizaji na dhulma za kimfumo dhidi ya Wapalestina ni mwingi sana, na habari za dhulma hizo hazipaswi kufichwa tena.

Vilevile wameashiria ripoti yenye kurasa 213 iliyochapisha na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch tarehe 27 Aprili kuhusu jinai za ubaguzi wa Apartheid na dhulma za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusema: "Ripoti hiyo imesajili uhalifu na jinai nyingi dhidi ya binadamu zilizofanywa na Israel katika fremu ya siasa za ubaguzi wa rangi wa Apartheid."  

Tags