Jun 14, 2021 04:51 UTC
  • Nchi tajiri duniani zakataa kudhamini chanjo ya kutosha ya COVID-19 kwa nchi masikini

Katika hali ya sasa ambapo ugonjwa wa COVID-19 unaendelea kusababisha maafa duniani na kuwaathiri vibaya watu wengi hasa katika nchi maskini, inasikitisha kuona usambazwaji usio wa kiadilifu wa chanjo ya COVID-19 ukiendelea kuzisumbua na kuzitia mashakani nchi mbalimbali.

Wataalamu wanashauri kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa kimataifa ili nchi maskini na dhaifu nazo ziweze kupata chanjo ya COVID-19 na hatimaye kuangamiza kikamilifu janga hilo. Hata hivyo nchi tajiri duniani zimekaidi ushauri huo na katika hatua ya hivi karibuni kabisa, viongozi wa nchi wanachama wa kundi la G7 wamepinga pendekezo la kutenga bajeti maalumu ya kudhamini mahitaji yote ya chanjo ya COVID-19 kwa ajili ya nchi maskini.

Viongozi wa nchi tajiri kiviwanda maarufu kama G7 ambazo ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani, wamekutana London ambapo ajenda muhimu katika kikao hicho ilikuwa janga la COVID-19. Katika hali ambayo ilitarajiwa viongozi wa nchi hizo wangeafiki kudhamini mahitaji ya dozi za chanjo ya COVID-19 kwa ajili ya nchi maskini na dhaifu lakini waliahidi kutoa dozi bilioni moja tu kwa nchi hizo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, imepengwa kuwa dozi milioni 200 zitakabidhiwe nchi maskini kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2021. Gazeti la Independent la Uingereza limeandika kuwa, nchi za G7 hazikujadili uwezekano wa kuzipa msaada wa kifedha nchi maskini na zilijikita tu katika kadhia ya chanjo ya COVID-19 ambapo jumla ya dozi ambazo zimeahidiwa katika kikao hicho zitakidhi asilimia 10 tu ya mahitaji ya nchi maskini.

Chanjo ya COVID-19

Hatua hiyo ya nchi za G7 imechukuliwa katika hali ambayo hivi karibuni viongozi 100 wa zamani duniani wakiwemo waliowahi kuwa marais, mawaziri wakuu na mawaziri wa mambo ya nje waliandika barua na kuzitaka nchi hizo tajiri kiviwanda kulipa gharama za kuwapa chanjo ya COVID-19 watu wote duniani ili kuzuia kuibuka maafa makubwa zaidi. Walisisitiza kuwa janga la COVID-19 ni la kimataifa na kuna haja ya kuwepo ushirikiano ili kuangamiza janga hilo.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, zaidi ya watu milioni 176 kote duniani wameambukizwa COVID-19 na zaidi ya milioni tatu na lakini nane miongoni mwao wamepoteza maisha. Hali inaripotiwa kuwa mbaya katika nchi maskini hasa nchi za Afrika ambazo hazijapata chanjo ya kutosha.

John Nkengasong mkuu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) anasema bara la Afrika limegonga mwamba katika kukidhi mahitaji yake ya chanjo ya COVID-19.

Hata baadhi ya nchi ambazo zina fedha za kutosha za kununua chanjo ya COVID-19 hazijaweza kupata chanjo kutokana na uhaba wa chanjo. Hali hiyo inatokana na kuwa, nchi za Ulaya, Marekani na Canada si tu kuwa haziko tayari kutoa msaada wa kifedha kwa ajili ya kununua chanjo ya corona, bali hata zimejirundikia chanjo hiyo ya COVID-19 zaidi ya mahitaji yao.

Utendaji wa nchi hizo za Magharibi unaonyesha kuwa licha ya madai yao ya kutetea haki za binadamu na usawa, laiki hazijatekeleza nara hizo kivitendo bali zimenunua chanjo ziada na kuziweka katika maghala yao, na huo bila shaka ni ugaidi wa kimatibabu.

Ngozi Okonjo-Iweala mkuu wa Shirika la Biashara Duniani

Bi. Ngozi Okonjo-Iweala mkuu wa Shirika la Biashara Duniani anasisitiza kuwa, kufufua uchumi wa dunia kunategemea ni kiasi gani nchi mbalimbali zitakuwa zimepiga hatua katika kutoa chanjo ya COVID-19. Vilevile ametahadharisha kuwa, ukosefu wa chanjo ya corona unaweza kuzorotesha uchumi wa nchi za Amerika ya Latini na Afrika.

Maambukizi ya COVID-19 duniani yanaweza kudhibitiwa kwa ushirikiano wa kimataifa, na iwapo hakutakuwapo ushrikiano huo basi madhara yatazikumba nchi zote duniani. Umaskini hautakua na athari mbaya kwa nchi maskini tu bali kwa dunia nzima. 

Tags