Jun 17, 2021 03:37 UTC
  • Uzinduzi wa Stratijia ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi wa Ndani nchini Marekani

Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, Jumanne wiki hii ilizindua Stratijia ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi wa Ndani (National Strategy for Countering Domestic Terrorism) ambayo imetayarishwa na Baraza la Usalama wa Taifa. Kwa mujibu wa hati hiyo, taasisi zote za utekelezaji ndani ya Marekani zinalazimika kupambana na aina mbalimbali za ugaidi wa ndani ya nchi hiyo.

Hati hiyo imezungumzia jinsi ya kutambua ipasavyo makundi yenye misimamo mikali ya ndani ya nchi na hatua za kigaidi tangu zinapangwa hadi kutekelezwa. Vilevile imejumuisha njia za kuimarisha ushiriki wa sekta zote katika kutekeleza sheria na kuzuia usajili wa watu wenye misimamo mikali katika jeshi la Marekani. 

Shambulizi lililofanywa na wafuasi wenye misimamo ya kufurutu mipaka wa aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya majengo ya Kongresi tarehe 6 Januari mwaka huu wa 2021 ambao wengi wao ni wanamgambo wa makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, lilipelekea kumulikwa tena tatizo sugu la kustawi harakati za ugaidi wa ndani nchini Marekani. Januari mwaka jana Rais Joe Biden wa Marekani aliwataja wafuasi wa Donald Trump kuwa ni magaidi wa ndani ya nchi. Msimamo huo wa Biden ulitambuliwa kuwa na umuhimu mkubwa, kwa sababu ulikiri, ingawa kwa kuchelewa, kuhusu utambulisho wa kigaidi wa makundi ya mrengo wa kulia ya Marekani.

Kundi la kigaidi la Oath Keepers, Marekani

Wademokrati wengi walilitaja shambulizi dhidi ya majengo ya Kongresi kuwa ni ugaidi wa ndani na wametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu hujuma hiyo na kuchukua hatua ya kuzuia uwezekano wa kutokea tena katika siku za usoni. 

Ni kwa kutilia maanani ukweli huo na tathmini zilizofanywa kuhusu harakati za makundi mbalimbali yenye misimamo ya kufurutu mipaka ya mrengo wa kulia na wanamgambo ndani ya Marekani, ndipo White House ikachukua hatua ya kubuni na kuzindua Stratijia ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi wa Ndani. Hati hiyo imesisitiza kuwa, ugaidi wa ndani ya Marekani unastawi na kupanuka zaidi na kwamba unajumuisha sehemu kubwa ya makundi mengi yenye aidiolojia za kikatili, chuki za kikaumu na kimbari na vilevile uhasama dhidi ya serikali. Kuna makundi yenye misimamo mikali ya kuchupa mipaka nchini Marekani kuanzia makundi madogo ya upinzani hadi mitandao mikubwa inayolenga na kuhujumu baadhi ya jamii za nchi hiyo na yanayojitambua kuwa makundi ya wanamgambo wapinzani yenye lengo la kuvuruga nidhamu na utekelezaji wa sheria.

Rais Joe Biden wa Marekani ametoa taarifa akisema: "Hatuwezi kufumbia macho vitisho vinavyoongezeka kila siku vya kuzusha mizozo na mapigano ya ndani. Kuna ulazima wa Serikali ya Federali na viongozi wote wa Marekani kutoa jibu kwa tishio hilo."

Mtaalamu wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani, Seth Jones anasema: "Hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa kuhusu idadi kubwa ya njama na mashambulizi ya ugaidi wa ndani ikilinganishwa na miongo iliyopita. Ni muhimu sana kwa Marekani kutambua vyema jambo hilo kabla hali haijawa mbaya zaidi."

Wamarekani wenye misimamo mikali akivamia Kongresi

Mizizi ya ugaidi wa ndani huko Marekani inarejea katika miongo kadhaa iliyopita, na baadhi ya watu na makundi yanayopinga serikali yamekuwa yakijihusisha na vitendo vya kigaidi. Taarifa iliyotolewa na White House kuhusu uzinduzi wa Stratijia ya Taifa ya Kupambana na Ugaidi wa Ndani imesema: "Katika miaka ya karibuni Marekani imeonja mashaka na maumivu makubwa ya hujuma za ugaidi wa ndani. Vitendo vya ugaidi yakiwemo mashambulizi ya silaha vimeongezeka sana katika maeneo mbalimbali ya Marekani."

Sehemu kubwa ya ugaidi wa ndani nchini Marekani unafanywa na watu au makundi ya wanamgambo wenye mitazamo ya kihafidhina ya mrengo wa kulia. Kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani hapo mwaka 2016 kunatajwa kuwa chachu iliyohuisha harakati za makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka ya mrengo wa kulia. Vilevile mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kustawisha fikra za kuchupa mipaka za mrengo wa kulia.

Kwa sasa kumegunduliwa makundi zaidi ya 1,600 yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Marekani na muhimu zaidi kati ya makundi hayo ni "Proud Boys", "Oath Keepers" na "QAnon".    

Tags