Jun 17, 2021 07:34 UTC
  • Biden atafakari kuvirejesha vikosi vya Marekani nchini Somalia

Rais wa Marekani, Joe Biden anatafakari kuwarejesha wanajeshi wa nchi hiyo huko Somalia, eti kwenda kusaidia juhudi za kupambana na magaidi wa kundi la ukufurishaji la al-Shabaab.

Pendekezo la Biden la kutuma makumi ya askari wa Marekani nchini Somalia limefichuliwa na gazeti la New York Times ambalo limeandika kuwa, Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani hajapokea nakala la pendekezo hilo kufikia sasa.

Ikumbukwe kuwa, mtangulizi wa Biden, Donald Trump mwaka uliopita kabla ya kuondoka ofisini alitoa amri ya kuondolewa nchini Somalia kwa askari wanaokadiriwa kuwa 700 wa Marekani kufikia Januari 15 mwaka huu.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilisema wakati huo kwamba, wanajeshi hao watatumwa katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki, pengine Kenya au Djibouti; eti kuendeleza vita dhidi ya ugaidi.

Askari wa Marekani walipokuwa Somalia

Askari hao wa Marekani wamekuwepo nchini Somalia kwa kisingizio cha kuvisaidia vikosi vya serikali ya Mogadishu katika operesheni zake za kukabiliana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab. Hata hivyo wamekuwa wakilaumia kwa kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yao ya anga.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya utawala wa Biden kutangaza kuwa utatuma vikosi maalumu vya wanajeshi nchini Kenya, eti kwenda kusaidia juhudi za kupambana na magaidi wa kundi la ukufurishaji la al-Shabaab.

Tags