Jun 18, 2021 12:48 UTC
  • Ufaransa yaitumia Algeria chakula chenye mizoga ya nguruwe, Algiers yakirejesha kilikotoka

Waziri wa Kilimo wa Algeria amesema kuwa, Ufaransa imeitumia nchi yake chakula kilichooza na kilichomaliza muda wake. Chakula hicho kimegunduliwa baada ya kupatikana mizoga miwili ya nguruwe katika shehena ya ngano iliyoingizwa nchini humo kutoka Ufaransa.

Kitendo hicho cha kijinai cha mkoloni Ufaransa kimeikasirisha Algeria na kuamua kukirejesha haraka kilikotoka chakula hicho.

Waziri wa Kilimo wa Algeria, Abdelhamid Hamdani amenukuliwa na vyombo vya habari akionesha hasira zake kubwa kutokana na madharau hayo iliyofanyiwa Algeria na mkoloni Mfaransa na kusema kuwa, Paris lazima iilipe fidia Algeirs.

Shehena hiyo ni ya tani 27,000 za ngano na Ufaransa imetuma kiwango hicho kikubwa cha chakula kwa Algeria licha ya kwamba kimeshaoza na mpaka mizoga ya nguruwe imepatikana ndani yake.

Algeria ni mnunuzi mkubwa wa ngano, hata hivyo nchi kama Ufaransa inatumia vibaya fursa hiyo kuiuzia Algeria ngano iliyooza na iliyo na mizoga ya nguruwe

 

Mtandao wa habari wa Arabi 21 nao umethibitisha habari ya kupatikana mizoga miwili ya nguruwe ndani ya shehena mbili za ngano hiyo iliyotokana nchini Ufaransa. Tukumbuke kuwa katika kitu ambacho kila Muislamu anajiepusha nacho mno, ni nyama ya nguruwe, hatusemi tena mizoga yake tena iliyopatikana ndani ya chakula. 

Algeria ni moja ya wanunuzi wakubwa wa ngano duniani na sehemu kubwa ya mahitaji yake inanunua kutoka Ufaransa. Pamoja na hayo Paris bado inaamiliana kikoloni na Algeria na haijali hisia za Waislamu wa nchi hiyo.

Wiki iliyopita pia, Algeria ilikataa kupokea shehena ya tani 33,000 za ngano kutoka Canada kutokana na kutokuwa na viwango vya chakula salama kinachoweza kuliwa na mwanadamu. Hayo yaliripotiwa na kanali ya televisheni ya Ennahar ya Algeria.