Jun 20, 2021 02:23 UTC
  • Joe Biden
    Joe Biden

Mamia ya shakhsia wa kisiasa, wanaakademia, wanaharakati wa amani na washindi wa Tuzo ya Nobel wamemtaka Rais Joe Biden wa Marekani atimize ahadi yake ya kulinda haki za Wapalestina, na kukomesha dhulma za Israel.

Katika barua yao ya wazi, shakhsia na wanaharakati hao wa kisiasa na kijamii wamemtaka Biden kulifanya suala la haki za binadamu kuwa kitovu cha sera za mambo ya nje za Marekani.

Mamia ya shakhsia hao wa kisiasa, wanaakademia, wanaharakati wa amani na washindi wa Tuzo ya Nobel wamemhutubu Rais Joe Biden wa Marekani wakimuambia: Utawala wako unapaswa uweke mashinikizo ya kidiplomasia yanayosaidia kuhitimisha ubaguzi na dhulma zilizoratibiwa, na kuhakikisha kuwa watawala wa Israel wanaokanyaga haki za Wapalestina wanawajibishwa.

Wameutaka utawala wa Biden uchunguze chimbuko na mzizi wa migogoro katika eneo la Asia Magharibi, ambayo tawala zilizopita zilipuuza.

Hujuma za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Ikumbukwe kuwa, Wapalestina 253 waliuawa shahidi katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko katika Ukanda wa Gaza mwezi Mei mwaka huu.

Watoto 66, wanawake 39 na wazee 17 ni miongoni mwa raia wa Palestina waliouliwa shahidi katika vita hivyo vya Israel, huku wengine zaidi ya 1900 wakijeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama dhidi ya Gaza. 

Tags