Jun 20, 2021 13:21 UTC
  • Abbas Araqchi
    Abbas Araqchi

Mwakilishi mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia amesema sasa ni wakati pande zingine katika mkataba wa nyuklia ya JCPOA kuchukua maamuzi ya kuyahuisha mapatano hayo ya mwaka 2015 kwani nyaraka zote ziko tayari kwa ajili ya mapatano ya mwisho.

Akizungumza mjini Vienna, Austria kunakofanyika mazungumzo hayo, Abbas Araqchi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, "hivi sasa tumekaribia mapatano zaidi ya wakati wowote ule na kilichobakia ni pande zingine katika mazungumzo hayo kuchukua maamuzi."

Mzunguzmo hayo ya JCPOA mjini Vienna yanajumuisha Iran katika upande mmoja na upande wa pili unajumuisha nchi za P4+1 ambazo China, Russia, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.

Hizo ndizo pande zilizosalia katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa mwaka 2018.

Araqchi amesema leo Jumapili ni siku ya mwisho ya duru ya sita ya mazungumzo ya Vienna na sasa baada y mazungumzo magumu nyaraka zote ziko tayari kwa ajili ya mapatano.

Hatahivyo ameongeza kuwa bado kuna baadhi ya masuala ambayo hayajaweza kutatuliwa na ameelezea matumaini kuwa kutafikiwa muafaka wa mwisho katika mazungumzo. 

Araqchi pia ameonya kuwa ni vigumu kutabiri kitakachojiri katika siku za baadaye kwani mazungumzo yakimalizika wawakilishi wote watarejea katika nchi zao kwa mashauriano na maamuzi ya mwisho.

Mazungumzo hayo ya Vienna yalianza Aprili kwa lengo la kujadili njia za kuishawishi Marekani irejee katika mapatano ya JCPOA na iyatekeleza kikamilifu kwa kuondoa vikwazo vyote ilivyoweka dhidi ya Iran.