Jun 22, 2021 08:05 UTC
  • Siku ya Wakimbizi; kuzidi kuwa kubwa mgogoro wa jamii ya wakimbizi duniani

Tarehe 20 Juni katika kalenda ya Umoja wa Mataifa, ni Siku ya Wakimbizi ulimwenguni. Siku hiyo huadhimishwa kila mwaka kwa njia mbalimbali.

Wakimbizi ni sehemu muhimu na kubwa katika jamii ya mwanadamu duniani leo. Takwimu za karibuni kabisa zinaonesha kuwa, sasa hivi kuna zaidi ya wakimbizi milioni 82 katika kona mbalimbali za dunia. Idadi hiyo inaunda zaidi ya asilimia moja ya watu wote ulimwenguni na ni sawa na idadi ya watu wa nchi moja kubwa duniani.

Kiujumla kuna aina tatu za jamii ya wakimbizi duniani. Wakimbizi wa ndani ya nchi ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbalimbali. Idadi ya wakimbizi wa ndani kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa ni watu milioni 48.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, kila mwaka idadi ya wakimbizi inaongezeka duniani. Kwa kweli huu ni mwaka wa 9 mfululizo ambapo idadi ya wakimbizi inaongezeka na haipungui. Mwaka jana kwa mfano, na licha ya kuweko janga la corona lililozilazimisha nchi za dunia kuweka sheria kali za kusafiri ikiwa ni hatua kuu ya kukabilianaa na ugonjwa huo wa COVID-19 ulioenea dunia nzima, lakini pamoja na hayo, idadi ya wakimbizi iliongezeka kwa asilimia nne duniani.

Filippo Grandi,  Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi

 

Sababu kuu inayolazimisha watu wa jamii fulani kuhama nchi yao na kukimbilia nchi nyingine ni ukosefu wa usalama na amani katika maeneo yao. Wakimbizi milioni 2 na laki 3 wa ndani ya nchi waliongezeka katika jamii ya wakimbizi mwaka jana 2020. Wengi wa wakimbizi hao wa mwaka jana ni kutoka nchi za Ethiopia, Sudan, Msumbiji, Yemen, Afghanistan na Colombia.

Ijumaa wiki hii, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi, Filippo Grandi, alisema kuwa, licha ya mipaka ya nchi mbali mbali kufungwa na licha ya mataifa ya dunia kuweka sheria kali za kukabiliana na corona, lakini pamoja na hayo, masuala kama vita, machafuko na uvunjaji wa haki za binadamu hayajaruhusu kupungua idadi ya wakimbizi duniani.  Alisema, karibu watu milioni tatu walilazimika kukimbia makazi yao katika kona mbalimbali za dunia mwaka uliopita wa 2020 kutokana na vita, machafuko na uvunjaji wa haki za binadamu. Kwa mujibu wa kamishna huyo wa masuala ya wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, maeneo kama ya Msumbiji, Tigray Ethiopia na eneo la Sahel la Afrika. Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi, maeneo hayo aliyoyataja ndiyo yalikuwa wazalishaji wakubwa wa wakimbizi mwaka jana na kiujumla dunia ilishuhudia ongezeko la wakimbizi karibu milioni 3 mwaka huo.

Wakimbizi wa vita nchini Syria

 

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa,  hadi mwaka jana 2020, idadi ya wakimbizi duniani ilikuwa ni zaidi ya milioni 5 na laki 7 wa Kipalestina, milioni 3 na laki 9 wa Venezuala, milioni 20 na laki 7 wa nchi nyingine duniani, wote hao wanaishi nje ya mipaka ya nchi zao. Ripoti hiyo hiyo ndiyo iliyosema kuwa, hadi mwaka jana kulikuwa na wakimbizi milioni 48 wa ndani ya mipaka ya nchi zao.

Wanawake na watoto wadogo ndio wanaounda asilimia kubwa ya wakimbizi. Watu hao ni wahanga wakuu wa udhalilishaji wa kijinsia, magendo ya binadamu, kufanywa watumwa, kutumiwa na magenge ya ya kigaidi na yenye silaha yanayofanya machafuko kwa maslahi yao binafsi. Umoja wa Mataifa unasema, wakimbizi hao wanahitajia mno misaada ya kifedha na kudhaminiwa usalama wao, kwani miongoni mwa sababu za kuwa wakimbizi ni matatizo ya fedha na kukosekana usalama hata wa chakula katika maeneo yao.

Licha ya kuweko hali mbaya kiasi chote hicho ya wakimbizi duniani, lakini madola makubwa yanayojigamba ni watetezi wa haki za binadamu na walinzi wa amani na usalama duniani hayachukui hatua yoyote ya kuwasaidia watu hao au kupunguza wimbi la kuongezeka idadi ya wakimbizi ulimwenguni kwa muongo mzima sasa.

Tags