Jun 22, 2021 10:56 UTC
  • Human Rights Watch yakosoa ripoti ya Guterres kuhusu wakiukaji wa haki za watoto duniani

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limikosoa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kwa kutoyaweka majina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wakiukaji wakubwa wa haki za watoto duniani.

Mkurugenzi wa kitengo cha kulinda watoto katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Jo Becker amesema kuwa, watenda jina duniani wanaendelea kuua watoto na mabarobari kwa uungaji mkono wa Antonio Guterres. 

Becker ameongeza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaokoa na kuwapa kinga watu wanaofanya mauaji na ukatili unaowafanya vilema mamilioni ya watoto kwa kutoyaweka majina ya Saudi Arabia na Utawala wa Kizayuni wa Israel katika orodha ya fedheha ya wakiukaji wa haki za watoto duniani. 

Mkurugenzi wa kitengo cha kulinda watoto katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kutotayarisha ripoti sahihi ya wakiukaji halisi wa haki za watoto kwa mujibu wa ushahidi uliokabidhiwa kwa umoja huo ni kuwasaliti watoto na itahamasisha ukwepaji wa adhabu na uwajibishwaji.

Jo Becker amemtaka Antonio Guterres kutupilia mbali mwenendo huo wa kuwakingia kifua wahalifu hususan baada ya kuchaguliwa tena kuongoza Umoja wa Matafa kwa kipindi cha pili. 

Antonio Guterres

Awali Harakati ya Kimataifa ya Kutetea Watoto (World Movement for the Defense of Children) ilikuwa imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi watoto 2,100 wa Kipalestina katika kipindi cha baina ya mwaka 2000 hadi 2020. 

Katika ripoti ya hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliitaka Israeli kupunguza mashambulizi ya jeshi dhidi ya watoto wa Palestina na kuhakikisha adhabu inatolewa kwa wanajeshi wake wanaouawa watoto. Hata hivyo Antonio Guterres aliamua kutoliweka jina la Israel katika orodha ya makundi na tawala zinazokiuka haki za watoto licha ya kuua makumi ya watoto wadogo wa Palestina.