Jun 23, 2021 02:23 UTC
  • Undumilakuwili wa Marekani katika vikwazo; tangu madai ya kutokuwepo vikwazo vya dawa hadi kutoa ruhusa ya kufutwa vikwazo

Kwa miaka mingi sasa Iran iko chini ya mashinikizo ya chakula na madawa huku dola la kibeberu la Marekani likiendesha propaganda nyingi za uongo kuhusu suala hilo.

Kwa kawaida na kibinadamu, vikwazo havipaswi kuingia kwenye masuala ya afya, dawa na chakula, lakini kwa miaka mingi sasa Iran haiwezi kupata kiurahisi dawa wala kunufaika inavyotakiwa kimataifa katika masuala ya tiba na matibabu, kutokana na matatizo ya fedha za kigeni na kibenki yaliyosababishwa na vikwazo hivyo.

Hivi karibuni Wizara ya Hazina ya Marekani ilidai kuwa eti imeondoa marufuku ya kuamiliana na Iran katika mabadilishano ya dawa na vifaa vya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. 

Sehemu nyingine ya ruhusa hiyo ya Wizara ya Hazina ya Marekani imesema: "Mabadilishano na shughuli zote zinazohusiana na kusafirisha nje, soko la bidhaa za kigeni, mauzo na manunuzi, miamala mubashara na isiyo mubashara, iwe ya bidhaa au teknolojia bali kila kitu kinachotumika kwenye kuzuia, kugundua na kutibu ugonjwa wa COVID-19 kati ya Iran na pande nyingine au kati ya serikali ya Iran na upande wowote ule au baina ya watu wa kawaida na nchi ya tatu wanaonunua bidhaa za aina hiyo kwa ajili ya Iran, vyote hivyo sasa vinaruhusiwa na ni huru kuvifanya."

Wizara ya Hazina ya Marekani

 

Siku ya Jumapili, Kamati ya Haki Binadamu wa Idara ya Mahakama ya Iran ilijibu hatua hiyo ya Marekani ya kuiondolea vikwazo Iran vinavyohusiana na corona, kwa kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Wairan 82,000 wamefariki dunia kutokana na corona na baada ya kupita miezi 16 tangu kuanza janga la corona na wakati tayari Iran imeshajitengenezea chanjo yake ya kujikinga na ugonjwa huo, ndipo Marekani inajifanya kuondoa marufuku hiyo."

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Twitter wa kamati hiyo imesema: Linachotaka taifa la Iran ni kuondolewa vikwazo haramu na kuadhibiwa walioviweka, kwani vikwazo vyao ni kinyume cha sheria za kimataifa hata katika kipindi cha vita.

Upungufu wa madawa nchini Iran uliosababishwa na vikwazo vya Marekani unawadhuru watu wa kawaida wenye magonjwa tofauti humu nchini. Watoto wadogo wanaoteseka kwa saratani, wagonjwa wa maradhi sugu na wagonjwa waliathiriwa na mashambulizi ya silaha za kemikali ambazo Marekani na nchi za Ulaya zilimpa Saddam wakati wa vita ambavyo Iran ililazimishwa kupigana na utawala wa zamani wa Iraq, ndio wanaoathiriwa zaidi na vikwazo hivyo vya mabeberu.

Taifa la Iran limesimama imara kukabiliana na vikwazo vya madhalimu

 

Baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa kulalamikia jinai hizo, majaji wa mahakama hiyo walitoa hukumu ya kusema kuwa, wana haki ya kufuatilia mashtaka ya Iran dhidi ya Marekani kutokana na Washington kukanyaga makubaliano yanayohusiana na uhusiano wa kiuchumi na kisheria ya mwaka 1955. Majaji hao walitoa hukumu ya kuondolewa vikwazo vyote vya dawa, chakula, masuala ya kibinadamu na vya anga vilivyowekwa na Washington dhidi ya Tehran. Hata hivyo hadi hivi sasa Marekani inaendelea kufanya ukaidi na haitaki kutekeleza amri hiyo ya mahakama ya kimataifa.

Javid Montazeran, mtaalamu na mtafiti wa masuala ya sheria za kimataifa anasema: Kwa kitendo chake cha kufanya ukaidi na kukataa kutekeleza amri ya Mahakama ya Kimataifa kuhusu kuiondolea vikwazo Iran, Marekani imeonesha wazi kuwa haiko tayari kutekeleza kivyovyote vile amri hiyo ya muda ya Mahakama ya Kimataifa.

Kwa upande wake, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo yanayohusiana na utekelezaji sahihi na kamili wa makubaliano ya JCPOA ya huko Vienna Austria ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba: Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Marekani ilimuwekea vikwazo kila Muirani popote pale alipo. Vikwazo hivyo ni vya kinyama na ni kinyume sheria.

Naibu huyo wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameandika: Serikali ya hivi sasa ya Marekani nayo ni mshirika wa jina dhidi ya binadamu.