Jun 23, 2021 07:59 UTC
  • New York Times yafichua uhusiano wa wauaji wa Khashoggi na serikali ya Marekani

Vyobo vya habari vya Marekani vimefichua kuwa, Wasaudia wanne walioshiriki katika mauaji ya 2018 ya mwandishi wa habari wa Washington Post, Jamal Khashoggi, walipata mafunzo ya kijeshi huko Marekani mwaka uliotangulia chini ya kandarasi iliyoidhinishwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo.

Gazeti la New York Times limefuchua kuwa, mafunzo hayo ya kijeshi yalitolewa na kampuni ya masuala ya usalama ya Tier 1 Group iliyopo huko Arkansas inayomilikiwa na shirika la Cerberus Capital Management kwa shabaha eti ya kuwalinda viongozi wa Saudi Arabia. 

Habari hizi zimefichuliwa na vyombo vya habari vya Marekani baada ya safari ya Mkuu wa Shirika la Upepelezi la Misri Abbas Kamil kutembelea Washington ambako taasisi moja ya masuala ya sheria ya wajumbe wa Kongresi ilitaka kujadiliwa madai kwamba, Cairo ilihusika pia katika mauaji ya kigaidi dhidi ya Jamal Khashoggi. 

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa, maafisa wa serikali ya Saudi Arabia walioshiriki katika mauaji ya Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul hapo mwaka 2018 walipewa mada inayotumiwa kuua nchini Misri.

Ripoti zinasema taarifa hizo za kipelelezi zimepatikana baada ya kuwahoji baadhi ya maafisa wa Saudia walioshiriki katika mauaji ya mwandishi huyo wa habari. Ripoti hiyo inasema kuna uwezekano kwamba, baadhi ya Wamisri walishirikiana na Wasaudia katika mauaji hayo. 

Picha ya mwisho ya Jamal Khashiggi akiingia ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul

Jamal Khashoggi aliuawa kikatili na kisha mwili wake ukakatwa vipande vipande tarehe Pili mwezi Oktoba mwaka 2018 baada ya kuingia ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul, Uturuki. 

Saudi Arabia ilikaa kimya kwa siku 18 bila ya kusema lolote baada ya kujiri mauaji hayo ya kutisha hadi pale serikali ya Uturuki ilipotoa ripoti mbalimbali na Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilipothibitisha kuwa Khashoggi aliuawa kwa amri ya moja kwa moja kutoka kwa Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.