Jun 23, 2021 12:02 UTC
  • Pendekezo la Waziri Mkuu wa Pakistan la kumalizwa mgogoro wa miaka mingi wa Afghanistan

Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan ametoa pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu huyo wa Pakistan amesema, lililo muhimu kuliko jambo lolote huko Afghanistan ni kufikiwa mafahamiano ya kisiasa na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ili kuzuia kuendelea kumwagwa damu za watu wasio na hatia. Amesema, bila ya shaka yoyote, kundi la Taliban inabidi lipewe nafasi kwenye serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Mkuu huyo wa chama tawala cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) ameongeza kuwa, iwapo serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa huko Pakistan, jambo hilo litaweza kuleta matumaini mapya ya kukomeshwa machafuko na mauaji nchini humo.

Vile vile ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatari ya kuendelea mapigano ya wenyewe kwa wenye nchini Afghanistan na kusema kuwa, kama kundi la Taliban litaendelea na ndoto yake ya kuteka ardhi zote za Afghanistan, basi umwagaji mkubwa wa damu kitakuwa ni kitu kisichoepukika kabisa.

Kundi la Taliban linatumia mtutu wa bunduki kushinikiza ndoto zao Afghanistan

 

Pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa ajili ya kukomesha mapigano nchini Afghanistan ambalo limetolewa na waziri mkuu wa Pakistan, si mpango mpya wa utatuzi wa mgogoro wa Afghanistan. Huko nyuma pia mpango huo uliwahi kupendekezwa na si viongozi waliotangulia wa Pakistan tu, bali pia na viongozi wa nchi nyinginezo. Mara zote serikali ya Afghanistan imekuwa ikipokea kwa jicho zuri mpango wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kushirikishwa wapinzani likiwemo kundi la Taliban.

Mpango wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Afghanistan una maana ya kuondolewa baadhi ya madaraka ya nchi mikononi mwa serikali na kupewa wapinzani likiwemo kundi la Taliban. Serikali ya nchi hiyo imekubali kwani inasema, inaumizwa sana na mateso wanayoendelea kupata Waafghani, na kuna haja ya kupatikana haraka utulivu nchini humo. Vile vile serikali hiyo haifichi kuonesha hisia zake za kuchoshwa na mgogoro wa miongo miwili sasa hata hivyo inachosisitiza serikali ya Afghanistan ni kuchungwa demokrasia na mfumo wa Jamhuri wa kuheshimiwa maamuzi ya wananchi.

Hata hivyo kuna vizuizi mbalimbali vinavyokwamisha mpango huo wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Mosi ni aidiolojia ya kundi la Taliban ambalo linaamini kuwa, wananchi hawapaswi kupewa nafasi ya kuchagua viongozi wao, bali mtawala mmoja mwenye nguvu inabidi atawale katika nchi na yeye ateuwa magavana na maliwali wake katika majimbo tofauti ya nchi. Upande wa serikali ya Afghanistan lakini unasema kuwa, maamuzi ya wananchi ni jambo la dharura. Kuendelea demokrasia ya mfumo wa Jamhuri unaoheshimu maamuzi ya wananchi ni jambo lisiloepukika. Serikali hiyo pia imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa, kuingizwa serikali kundi la Taliban bila ya ridhaa ya wananchi, ni jambo lisilokubaika. Msimamo wa serikali ya Afghanistan ni kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kama wananchi watachagua kutawaliwa na kundi la Taliban, kundi hilo likabidhiwe madaraka bila ya pingamizi yoyote. Serikali ya Afghanistan inasisitizia kuheshimiwa katiba ya nchi hiyo na inaamini kwamba si sahihi kumpokonya madaraka mtu aliyechaguliwa kidemokrasa na kumpa madaraka hayo mtu aliyetumia mtutu wa bunduki kinyume na ridhaa ya wananchi.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan

 

Rais Mohammad Ashraf Ghani wa Afghanistan mara chungu nzima amekuwa akitangaza kuwa, serikali yake haina tatizo lolote la kushirikishwa wapinzani likiwemo kundi la Taliban katika madaraka, muhumu tu sheria zifuatwe na katiba iheshimiwe. Hata amekuwa akitangaza kuwa yuko tayari kujiuzulu na kumkabidhi madaraka mtu yeyote atakayechaguliwa na wananchi kwa mujibu wa katiba.

Inaonekana wazi kwamba, kundi la Taliban haliko tayari kukubali utatuzi huo kwani kuna uwezekano wananchi wasiwape kura zao wanachama wa kundi hilo, na ndio maana inapata nguvu fikra kwamba kundi la Taliban litaendelea kushikilia ndoto yake ya kuteka ardhi zote za Afghanistan kwa mtutu wa bunduki.

Tags