Jun 26, 2021 12:42 UTC
  • Palestina, OIC zailaani Honduras kwa kuuhamishia ubalozi wake Quds

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imekosoa vikali hatua ya serikali ya Honduras ya kuuhamishia ubalozi wake Quds Tukufu kutoka Tel Aviv.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema hatua hiyo ya serikali ya Honduras ya kupuuza azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juu ya mji huo mtukufu ni jambo la kufedhehesha na kinyume cha sheria.

Taarifa hiyo imesema hatua ya Honduras inaenda kinyume na makubaliano ya mwaka 2011 ya viongozi wa Amerika ya Kati, ya kuitambua Palestina kama taifa huru, mji mkuu wake ukiwa Quds.

Nayo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imesema hatua hiyo ya serikali ya Honduras imepuuza azimio nambari 478 (1980), la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kwa msingi huo imekanyaga sheria za kimataifa.

Katibu Mkuu wa OIC ameitaka nchi hiyo ya Amerika ya Latini iangalie upya uamuzi wake huo, akisisitiza kuwa jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuongeza jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Palestina-Israel kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imelaani hatua hiyo ya Honduras kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv, kwenda mji wa Quds (Jerusalem), na kusisitiza kuwa na kusisitiza kuwa ni kinyume na sheria za kimataifa.

Ikumbukwe kuwa, Disemba mwaka 2017 aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa Washington inaitambua Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel na kisha kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv. 

Baadhi ya nchi kama Kosovo, Guatemala na Paraguay zimefuata kibubusa sera za Washington na kuafiki suala la kuhamisha balozi zao kutoka Tel Aviv kwenda mji wa Quds, kitendo ambacho kinakiuka sheria za kimataifa. Hata hivyo Paraguay ilifutilia mbali uamuzi huo miezi minne baadaye.

Tags