Jul 24, 2021 14:48 UTC
  • HRW: Biden anapaswa kusitisha uuzaji wa silaha kwa tawala zinazokiuka haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Righs Watch limemtaka Rais Joe Biden wa Marekani asitishe uuzaji wa silaha kwa wakiukaji wa haki za binadamu zikiwemo tawala za Misri na Israel.

Katika makala yake iliyochapishwa kwenye gazeti la Washington Post, mwakilishi wa Human Righs Watch mjini Washington, Alyssa Epstein ameashiria kuwa, mwezi Juni mwaka huu serikali ya Biden ilituma taarifa kwenye Kongresi ikiitarifu kwamba, ina nia ya kuiuzia Ufilipino silaha zenye thamani ya dola bilioni 2.5 na kuongeza kuwa, muamala huo wa kibiashara unakiuka ahadi ya Biden na waziri wake wa mambo ya nje, Antony Blinken kwamba serikali mpya ya Marekani italipa kipaumbele suala la haki za binadamu katika siasa zake za nje.

Epstein amesema: "Ni wazi kwamba serikali ya Joe Biden ina nia ya kuziuzia silaha tawala tatu zinazokanyaga haki za binadamu ambazo ni Ufilipino, Misri na Israel. Huu ni ukiukaji wa ahadi yake ya kutanguliza mbele haki za binadamu katika siasa zake za nje." 

Hii si mara ya kwanza kwa Joe Biden kukosolewa kwa kuziuzia silaha tawala kandamizi na zinazokiuka haki za binadamu katika kipindi kifupi cha utawala wake. Mwezi Februari mwaka huu wa 2021 Washington ilipasisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 197 kwa serikali ya Misri. Mwezi Mei pia, wakati wa mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina, Marekani iliidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 735 kwa utawala katili wa Israel. Silaha kama hizo za Marekani pia zimekuwa zikitumiwa katika mashambulizi ya kinyama ya utawala huo ghasibu dhidi ya watu wa Gaza na kwa ajili ya kuharibu makazi ya raia wasio na hatia na miundomsingi ya Wapalestina. Aghlabu ya silaha zilizouzwa na Marekani kwa Israel ni zile za Joint Direct Attack Munitions (JDAM). Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umenunua kiwango kikubwa cha siaha za aina hiyo umetangaza kwamba, umezitumia dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana baadhi ya wawakilishi katika Kongresi ya Marekani wakakosoa hatua ya serikali ya Joe Biden ya kuidhinisha mauzo ya silaha kwa Israel na kusema kuwa, suala hilo linazidisha mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Palestina.

Watoto wa Gaza waliouawa kwa mashambulizi ya Israel

Mbunge wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani, Ilhan Omar, anasema: "Hatua ya serikali ya Biden ya kuidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 735 kwa Israel inaaibisha. Mkataba huo wa silaha ni sawa na kubariki ukati wa Israel."  

Taarifa ya Human Rights Watch imetaja baadhi tu ya majina ya tawala ambazo serikali ya Biden imeziuzia silaha licha ya rekodi yao mbaya ya haki za binadamu. Mfano mwingine wa jambo hilo ni hatua ya serikali ya sasa ya Marekani kuendelea kuiuzia silaha serikali ya kifalme ya Saudi Arabia inayojulikana kwa rekodi mbaya na ya kutisha ya kukanyaga haki za binadamu.  

Awali serikali ya Biden ilidai kuwa, itatazama upya uhusiano wa Washington na Riyadh na kuchukua hatua kali dhidi ya utawala huo hususan katika suala la mauzo ya silaha. Hata hivyo maslahi ya muda mrefu ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia yameifanya serikali ya Biden ibadili msimamo wake kuhusu Saudia, na maslahi ya kiuchumi, kisiasa na kistratijia yameipelekea Marekani ianze kuhuisha tena uhusiano wake wa kijadi na utawala wa ukoo wa Aal Saud ikiwa ni pamoja na kurusu mauzo ya silaha kwa utawala huo.

Kulegeza kamba kimyakimya Marekani katika uhusiano wake na Saudi Arabia licha ya utawala huo kukosolewa kimataifa kutokana na mauaji yanayoendelea kufanywa na Riyadh na washirika wake huko Yemen, kumefanyika licha ya Joe Biden kutangaza kuwa Washington imesimamisha mauzo ya silaha kwa utawala huo. Biden alitangaza waziwazi kuwa: “Marekani kamwe haitatupilia mbali misingi yake kwa ajili tu ya kununua mafuta na kuuza silaha!”

Watoto wa Yemen ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia

Sasa Marekani imeanza tena kuwauzia silaha za aina mbalimbali waitifaki wake wa kanda ya Magharibi mwa Asia kama Saudi Araba na Imarati. Hii ina maana kwamba, licha ya madai ya Washington ya eti kutetea haki za binadamu, lakini maslahi ya kifedha yanayotokana na ununuzi wa mafuta ya bei rahisi na mauzo ya silaha kwa tawala kama Saudi Arabia ndivyo vinavyoongoza na kuainisha uhusiano wa Washington na nchi hizo zinazojulikana kwa ukandamizaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Tags