Jul 25, 2021 01:20 UTC
  • Ilhan Omar ataka ufafanuzi wa Biden juu ya shambulio la anga Somalia

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic amemuandikia barua Rais Joe Biden wa nchi hiyo, akitaka ufafanuzi na maelezo kuhusu shambulio la kwanza la anga lililofanywa na utawala wake nchini Somalia.

Ilhan Omar ameutaka utawala wa Biden utoe maelezo ya kina kuhusu uhalali na mantiki ya kutekelezwa hujuma hiyo ya anga Jumanne iliyopita, licha ya Ikulu ya White House kutangaza kuwa ina mpango wa kupunguza operesheni za aina hii.

Mwanasiasa huyo mwenye asili ya Somalia mbali na kutilia shaka uhalali wa hujuma hiyo, lakini amesisitiza kuwa Marekani inapaswa kutazama upya malengo na sera zake zinazofungamana na 'mapambano dhidi ya ugaidi' nchini Somalia. 

Mbunge huyo Muislamu wa Kongresi ya Marekani kadhalika katika barua yake hiyo, ameikosoa White House kwa kukataa kutekeleza ahadi iliyotoa, ya kuzipa fidia familia za raia waliouawa katika hujuma hizo za anga za Marekani nchini Somalia.

Muda mfupi baada ya barua ya mjumbe huyo wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kuwasili White House, jeshi la Marekani lilifanya shambulio la pili la anga nchini Somalia Ijumaa iliyopita kwa kutumia ndege isiyo na rubani. 

Drone ya Marekani

Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM mara kadhaa imekiri kuua raia wa Somalia na kusababishia wengine ulemavu wa daima katika hujuma zake za anga zinazodaiwa kulenga maficho ya wanamgambo wa al-Shabaab.

Hivi karibuni pia, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema jeshi la Marekani linaendelea kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Tags