Jul 25, 2021 11:13 UTC
  • Maduro aliagiza jeshi la Venezuela litoe jibu kali kwa chokochoko za Marekani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amelitaka jeshi la nchi hiyo lijiweka tayari na kutoa jibu kali kwa uchokozi na uvamizi wa aina yoyote wa Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Maduro ametoa agizo hilo baada ya Wizara ya Ulinzi ya Venezuela kuituhumu Washington kuwa imehujumu anga ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Vladimir Padrino Lopez, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesema ndege ya kijeshi aina ya C-17 ya Marekani siku ya Alkhamisi iliruka katika anga ya jimbo la Zulia la nchi hiyo kinyume cha sheria, ikitokea Colombia.

Shirika la habari la Russia Today limeinukuu serikali ya Caracas ikisema kuwa Marekani imekiuka anga ya Venezuela mara zaidi ya 20 ndani ya mwaka huu pekee 2021.

Wanajeshi wa Venezuela

Kufuatia chokochoko hiyo mpya ya watawala wa Washington, Rais Maduro amelitaka vikosi vya jeshi la Venezuela kuwa macho na tayari kujibu chokochoko na uvamizi wowote wa Marekani.

Mbali na chokochoko hizo za kuhujumu anga, lakini Marekani imekuwa ikitangaza mara kwa mara vikwazo vya kiuchumi na kuchochea na kusaidia uharibifu wa miundombinu na wa kisiasa ndani ya Venezuela; dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia kwa sababu tu serikali hiyo haitaki kuburuzwa na dola la kibeberu la Marekani na inapigania ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Tags