Jul 25, 2021 11:20 UTC
  • Maelfu waandamana katika nchi za Magharibi kupinga chanjo ya lazima ya Corona

Maelfu ya watu wameendelea kuandamana kwa siku kadhaa sasa katika baadhi ya nchi za Magharibi kupinga sheria kali za kudhibiti msambao wa virusi vya Corona na vile vile kulalamikia hatua ya serikali za nchi hizo kuwalazimisha wananchi kupiga chanjo ya ugonjwa wa Covid-19.

Hapo jana maandamano makubwa yalishuhudiwa katika nchi za Australia, Italia, Ufaransa na Uingereza kupinga hatua ya kufungwa upya nchi hizo kwa ajili ya kudhibiti msambao wa kirusi cha Delta kinachoripotiwa kusambaa kwa kasi katika nchi nyingi duniani hivi sasa.

Kadhalika waandamanaji hao hususan katika nchi za Ulaya wamepinga mpango wa serikali za nchi hizo kuwalazimisha watu kupigwa chanjo ya Corona kwa kutumia mbinu mbali mbali.

Nchini Ufaransa, watu 160,000 wanaripotiwa kuandamana Paris na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo kupinga mpango wa serikali ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo, ya kuwalazimisha watu wote kupigwa chanjo ili wapewe 'pasi za afya' za kuruhusiwa kuendelea kufanya kazi na kuingia katika maeneo ya umma.

Kadhalika  maelfu ya watu wameandamana katika miji ya Rome, Naples na Turin huko Italia kupinga mpango kama huo, ambapo waliopigwa chanjo wanapewa 'pasi za kijani' na wale ambao hawajapigwa wanazuiwa kuingia katika majengo ya biashara, mahoteli na maeneo mengine ya umma.

Waandamanaji wakikabiliana na maafisa usalama Italia

Maandamano kama haya yameshuhudiwa katika mji mkuu wa Uingereza, London ambapo waandamanaji wamesikika wakipiga nara za kutaka 'uhuru wa kijamii' wa kuamua iwapo wapigwe au wasipige chanjo hizo.

Katika mji wa Sydney nchini Australia, waandamanaji wamekabiliana na maafisa usalama ambao wametumia mabomu ya kutoa machozi ili kuzima maandamano ya kupinga tangazo la kufungwa nchi. Makumi wametiwa mbaroni kwa kushiriki maandamano hayo katika majimbo ya New South Wales, Melbourne na vile vile jijini Sydney. 

Tags