Jul 26, 2021 08:02 UTC
  • Robert Malley
    Robert Malley

Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran amekiri kuwa vikwazo vya kidhulma na mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya nchi hiyo dhidi ya Iran yamefeli vibaya na amekariri madai ya kila siku ya serikali ya Joe Biden kuwa eti Washington iko tayari kurejea katika mapatano ya JCPOA iwapo Iran itatekeleza majukumu yake.

Bila ya kuashiria hatua ya Washington ya kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo, Robert Malley amedai kuwa: Washington imeeleza waziwazi kwamba ipo tayari kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuondoa vikwazo iwapo Iran itatekeleza majukumu yake ya kinyuklia. 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani ameongeza kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi yaliyotekelezwa na serikali ya Donald Trump dhidi ya Iran yamefeli pakubwa na hii imeathiri vibaya maslahi ya Marekani. 

Hata hivyo Robert Malley amesema Marekani haitaondoa vikwazo vyote ambavyo viliwekwa na serikali ya Trump dhidi ya Iran.

Maafisa wa Marekani wamekuwa wakikariri kwamba vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya nchi hiyo dhidi ya Iran yamefeli lakini hadi sasa hawajachukua hatua ya maana ya kivitendo ya kufuta vikwazo hivyo na kurejea kwenye mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA. 

Tarehe 8 Mei mwaka 2018 serikali ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ilikiuka majukumu yake na azimio la Umoja wa Mataifa na kujiondoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo ya nyuklia.  

Tags