Jul 30, 2021 07:17 UTC
  • Kuendelea kuboronga katika uzungumzaji kwazidi kutilia shaka uwezo wa kiakili wa Rais wa Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani ameboronga tena katika uzungumzaji na kuonyesha udhaifu wa kiakili wa kuhifadhi mambo alipoeleza kwamba, kulikuwa na sababu tatu zilizomfanya agombee urais, lakini katika kubainisha sababu hizo akataja sababu mbili tu.

Biden aliibuka na uborongaji huo mwingine mpya siku ya Jumatano alipotembelea kiwanda kimoja katika jimbo la Pennsylvania, ambapo alisema kulikuwa na sababu tatu ambazo zilimfanya agombee urais wa Marekani, lakini katika maelezo yake alizitaja mbili tu.

Rais huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 78 alijikanganya pia katika hotuba yake hiyo alipomtaja aliyekuwa rais wa nchi hiyo Barack Obama wakati madhumuni yake yalikuwa ni kumtaja mtangulizi wake Donald Trump, lakini akasahihisha haraka kauli yake.

Biden, ambaye ni maarufu pia kwa kutamka maneno kimakosa amekuwa akifuatiliwa sana na vyombo vya habari na kukosolewa na kufanyiwa istihzai na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Kula mwereka zaidi ya mara moja wakati akipanda ndege kumetilia shaka hata uwezo wa kimwili wa Biden

Video mbali mbali zinazomuonyesha Joe Biden akiboronga katika uzungumzaji tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani, ikiwemo kuyasahau majina ya maafisa wa serikali yake katika vikao na waandishi wa habari, zimezidi kutilia nguvu shaka iliyopo kuhusu uwezo wa kiakili na kimwili wa kiongozi huyo.

Katika kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari, Joe Biden alilitaja kimakosa jina la rais wa Afghanistan alipolitamka Kiyani badala ya Ashraf Ghani.../