Jul 31, 2021 13:38 UTC
  • HRW: Jeshi la Myanmar limetenda jinai dhidi ya binadamu tangu lifanye mapinduzi na kutwaa madaraka

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, jeshi la Myanmar limetenda jinai dhidi ya binadamu tangu lilipofanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi miezi sita iliyopita.

Taarifa ya Shirika la Human Rights Watch imesema kuwa, jeshi la Myanmar limefanya mauaji, mateso na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wanaopinga hatua ya jeshi ya kutwaa madaraka ya nchi kwa nguvu.

Brad Adams, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Human Rights Watch Kanda ya Asia amesema kuwa, hakuna mazunguzmo huku damu ikiendelea kumwagwa. Aidha amesema, vitendo vya jeshi la Myanmar ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na jinai dhidi ya binadamu na wahusika wanapaswa kushtakiwa.

Hivi karibuni Kamati ya Watoto ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, watoto wasiopungua 75 wameuawa nchini Myanmar na watu wapatao 1,000 wanashikiliwa kizuizini tangu jeshi la nchi hiyo lilipotwaa kwa nguvu madaraka ya nchi miezi kadhaa iliyopita.

Maandamano ya wananchi wa Myanmar ya kupinga jeshi kutwaa madaraka ya nchi

 

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.