Aug 02, 2021 03:56 UTC
  • Silaha zawa adimu kupatikana Marekani kutokana na kukithiri mno idadi ya wanunuzi

Marekani inakabiliwa na uhaba wa silaha kufuatia kuongezeka kwa kiwango kikubwa mno ununuzi wa silaha katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, kutokana na kuongezeka mno mahitaji ya raia wanaotaka kumiliki silaha katika miji mbalimbali ya Marekani, sambamba na usambaaji wa virusi vya corona nchini humo, silaha zimekuwa adimu na kusababisha matatizo pia kwa askari polisi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kufuatia usambaaji mkubwa wa virusi vya corona, machafuko ya kijamii na kuongezeka mno vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha nchini Marekani, raia wa nchi hiyo wamelazimika kununua kwa wingi silaha na zana za kujihami.

Kanali ya televisheni ya ABC News na taasisi ya utafiti ya Hifadhi za Ukatili wa Utumiaji Silaha zimeripoti kuwa, matukio yasiyopungua 915 ya ufyatuaji risasi yalitokea katika wiki iliyoishia Julai 26 katika maeneo mbalimbali ya Marekani na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 430.

Inatabairiwa kuwa, 2021 itaweka rekodi mpya ya matukio hayo, kwa sababu tangu ulipoanza mwaka huu hadi sasa, idadi ya watu waliouawa katika matukio ya ukatili wa kutumia silaha imepindukia 24,000.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi, kuna silaha zipatazo milioni 270 hadi 300 nchini Marekani, ikimaanisha kwamba, takriban kila mtu mmoja anamiliki silaha katika nchi hiyo.

Kuwepo uhuru wa kutembea na silaha nchini Marekani kunasababisha kutokea kila siku matukio ya ukatili wa ufyatuaji risasi katika kila pembe ya nchi hiyo, ambayo mengi yao husababisha vifo vya watu. Pamoja na hayo, lobi za viwanda vya utengezaji silaha nchini Marekani zina nguvu na satua za kiasi ambacho, bunge la nchi hiyo hadi sasa halijawa tayari kuchukua hatua za kuwawekea raia mipaka ya kutembea na silaha.../

 

Tags