Aug 02, 2021 10:26 UTC
  • Russia: Hakuna mbadala wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao huko Vienna nchini Austria amesema njia pekee ya kuyahuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuyarejesha katika hali yake ya asili.

Mikhail Ulyanov amesema hayo leo Jumatatu katika mahojiano na gazeti la Russia la Izvestia na kusisitiza kuwa, JCPOA haina chaguo mbadala na kwamba dhana na wazo la kutaka kuandikwa upya mapatano hayo ni njozi.

Ulyanov amebainisha kuwa, Russia inataka kuona makubaliano hayo ya kimataifa yanarejea katika hali yake ya mwanzo, pasi na kupunguzwa au kuongezewa kitu chochote.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia ameeleza bayana kuwa, tarehe ya kurejelewa tena mazungumzo ya Vienna ya kuhuisha mapatano ya JCPOA haijabainika, lakini hakuna shaka kuwa vikao hivyo vilivyosimamishwa tokea Juni 20, vitaendelea baada ya Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuapishwa.

Mapatano ya JCPOA yalianza kuyumba baada ya US kujiondoa kwayo kinyume cha sheria

Serikali mpya ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Joe Biden imekiri kufeli sera za mashinikizo ya kiwango cha juu  za serikali ya kabla yake dhidi ya Iran. Biden ametangaza kuwa anataraji kuirejesha Washington katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini hadi sasa hajachukua hatua ya maana kuhusu suala hilo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake imesisitiza kuwa, itatekeleza tena majukumu yake kwa mujibu wa mapatano hayo ya nyuklia pale Marekani nayo itakapoiondolea nchi hii vikwazo na kujiridhisha na hatua hiyo. 

 

 

Tags