Aug 04, 2021 10:48 UTC
  • Juhudi za UN za kukabiliana na ubaguzi wa rangi duniani

Hatimaye na baada ya majadiiano ya miaka kadhaa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kuundwa Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Watu wa Asili ya Afrika.

Chombo hicho kitakuwa na jukumu la kutoa maagizo ya kitaalamu kwa ajili ya kushughulikia changamoto za baguzi wa rangi, propaganda chafu dhidi ya wageni na taasubi na chuki za kidini au kikaumu.

Azimio hilo lililopasishwa kwa kauli moja na wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa limelihimiza jukwaa hilo kuwa chombo cha kuboresha usalama na maisha ya watu wenye asili ya Afrika na kuwajumuisha kikamilifu katika jamii wanakoishi. 

Hatua hii ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imechukuliwa katika kipindi ambacho ubaguzi wa rangi umeendelea kuwa tatizo sugu na kubwa katika nchi za Magharibi. Katika nchi nyingi za Magharibi hususan Marekani raia weusi na kaumu za waliowachache zinaendelea kusumbuliwa na matatizo mengi. Kwa mfano tu, wakati kiwango cha wazungu wasio na ajira kikiwa karibu asilimia 5 tu uko Marekani, asilimia karibu 13 ya Wamarekani weusi wanasumbuliwa na ukosefu wa ajira. Kiwango cha mshahara wa mfanyakazi mweusi wa Marekani ni karibu asilimia 70 ya mshahara wa mzungu mwenye utaalamu na kazi sawa na ile ya Mmarekani mweusi.  

Kwa sasa ambapo virusi vya corona vingali vinachukua roho za watu wengi kote duniani, katika baadhi ya nchi za Magharibi kaumu za waliowachache zinabaguliwa hata katika utoaji wa chanjo ya virusi hivyo. Kwa mfano tu, katika Jimbo la Illinois huko Marekani peke yake Wamarekani weusi wanaunda asilimia 70 ya watu wote walioaga dunia kutokana na Covid-19. Gavana wa jimbo hilo anasema: "Suala hili linashtua, lakini halishangazi sana kwa kutilia maanani ukosefu wa usawa unaoshuhudiwa katika mfumo wa huduma za afya tuliouzungumzia sasa kwa miaka mingi." 

Hali hii ya ukosefu wa usawa na ubaguzi inashuhudiwa pia katika vyombo vya sheria na usalama katika nchi za Magharibi. 

Haujapita muda mrefu tangu baada ya mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu wa Marekani dhidi ya rais mweusi wa nchi hiyo, Gorge Floyd, yaliyozusha malalamiko mengi ndani na nje ya Marekani. Picha za tukio hilo ziliitumbukiza Marekani na dunia kwa ujumla katika mshtuko mkubwa na kuzusha wimbi la maandamano ya kudai haki za watu weusi kote duniani. Maandamano hayo yaliongozwa na harakati ya Black Lives Matter. Mhadhiri wa sheria na historia katika Chuo Kikuu cha Harvard, Annette Gordon-Reed ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Pulitzer anasema: "Suala la mbari nchini Marekani linaweza kufananishwa na mto wenye maji ya juu na kina kirefu. Kwa sasa Marekani inamulikwa sana kwa ubaguzi wa rangi. Kwa sababu tunashuhudia kupamba moto mitazamo ya makundi ya wabaguzi wa kizungu, suala ambalo kwa walimwengu lina maana na kukandamizwa watu weusi.”

Ubaguzi wa rangi pia ni tatizo kubwa katika nchi za Ulaya. Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia dhulma kubwa na vitisho vinavyowakabili watu weusi na Waislamu wanaonyimwa haki sawa na raia wengine katika nchi za bara hilo. Propaganda chafu dhidi ya Uislamu, kuwatuhumu Waislamu kuwa na magaidi na mienendo mibaya ya polisi dhidi ya kaumu za waliowachache kimbari na kidini, vinaongezeka na kushadidi siku baada ya nyingine.

Kwa sababu hiyo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuwa, wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na wana hadhi na haki sawa, na wana uwezo wa kushiriki katika ujenzi na ustawi wa jamii. Baraza hilo linasisitiza kuwa fikra yoyote ya mbari moja kuwa bora kuliko nyingine si sahihi katika mtazamo wa kisayansi, inalaaniwa katika upande wa maadili na si ya kiadilifu, bali ni hatari katika mtazamo wa kijamii.

Pamoja na hayo inaonekana kuwa, bado kuna njia ndefu hadi kutekelezwa kikamilifu maagizo hayo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusiana na tatizo la ubaguzi wa rangi duniani.  

Tags