Aug 05, 2021 07:07 UTC
  • Dmitry Polyansky
    Dmitry Polyansky

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amepinga tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Magharibi dhidi ya Iran kuhusu shambulizi lililolenga meli ya Mercer Street na kusema, taarifa hizo zinakinzana na zimetegemea dhana na tetetsi.

Dmitry Polyansky ambaye alikuwa kijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya iwapo Baraza la Usalama linapaswa kujadili madai ya kushambuliwa meli ya Mercer Street katika Bahari ya Oman au la, amesema kuwa, taarifa zilizotolewa na Israel na baadhi ya nchi kama Uingereza na Marekani zinakinzana kikamilifu na zimetegemea dhana na tetesi.  

Polyansky amesema kuwa, uchunguzi kuhusu suala hilo bado unaendelea lakini kuna taarifa nyingi za kukinzana ambazo zimetegemea dhana na tetesi tu, Russia inapinga kikamilifu taarifa hizo.

Ijumaa illiyopita kundi moja la wanajeshi wa Uingereza lilitoa taarifa fupi likidai kuwa meli moja ilishambuliwa Alkhamisi iliyopita katika maji ya Bahari ya Oman. Baada ya hapo Wizara ya Ulinzi ya Ulingereza ilitangaza kuwa, meli hiyo inamilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba ilishambuliwa ikiwa umbali wa kilomita 280 kutoka Bandari ya al Duqm nchini Oman. 

Masaa machache baadaye kampuni ya Zodiac Maritime inayomilikiwa na bilionea wa Kizayuni, Eyal Ofer ilitoa taarifa ikitangaza kuwa, meli ya Mercer Street inayomilikiwa na Israel imeshambuliwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani katika Bahari ya Oman. Kampuni hiyo ilisema kuwa mabaharia wawili wa meli hiyo wameuwa.

Akijibu tuhuma za Israel na Marekani dhidi ya Iran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saeed Khateebzadeh alisema jana Jumapili kwamba, hii si mara ya kwanza kwa utawala huo wa Kizayuni kutoa tuhuma kama hizo na kwamba ni mbinu inayotumiwa kwa muda mrefu na utawala huo ghasibu. Amesema tuhuma hizo zimetolewa katika fremu ya lobi iliyoajiriwa na inayojulikana ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Marekani. 

Vilevile mbunge wa zamani wa Israel, Taleb Abu Arar alisema, kuna uwezekano kwamba, Israel imehusika na mashambulizi yaliyolenga meli za kubeba mafuta katika bandari ya al Fujairah, na utawala huo na washirika wake wa kikanda wanafanya njama za kuvuruga usalama na kuzusha machafuko katika eneo hili.

Tags