Aug 06, 2021 02:24 UTC
  • Mgogoro wa wakimbizi; italia yataka kuitishwe kikao maalumu cha kutafuta suluhisho

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia ametoa wito wa kuitishwa kikao maalumu cha kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa wakimbizi na kugawana wakimbizi hao baina ya nchi za Ulaya kwa uadilifu.

Wito huo umetolewa kufuatia kushadidi mgogoro wa wakimbizi wanaoelekea barani Ulaya. Waziri huyo amesema, kwa wiki kadhaa sasa mamia ya wahajiri wamekuwa wakielekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania na kwamba wengi wao wanaingia Italia hususan katika kisiwa cha Lampedusa. 

Suala la wahajiri na wakimbizi limekuwa changamoto kubwa kwa nchi za Ulaya katika miaka kadhaa ya karibuni. Wimbi la wakimbizi kuelekea Ulaya limeshadidi zaidi miaka ya karibuni kutokana na ukosefu wa amani, vita na hali mbaya ya kiuchumi katika baadhi ya nchi za Afrika na Asia. Hata hivyo nchi za Ulaya zinazojinadi kuwa zinajali ubinadamu, zimekuwa zikifunga mipaka yao na hata kuwarudisha wakimbizi walikotoka au hata kuwaacha wakihangaika baharini. 

Wakimbizi katika maji ya Bahari ya Mediterania

Kutokana na nafasi yao maalumu na kukaribia sana Bahari ya Mediterania, nchi za Italia na Ugiriki zinatambuliwa kuwa kivuko kizuri zaidi cha wakimbizi kuelekea Ulaya. Japokuwa wimbi la wakimbizi kuelekea Ulaya lilipungua kidogo miezi kadhaa iliyopita kutokana na kupungua migogoro ya kisiasa katika nchi za Afrika na Asia baada ya kushadidi maambukizi ya virusi vya corona, lakini sasa hali ya mambo imebadilika na kunashuhudiwa tena wimbi jipya la wakimbizi kuelekea kwenye mipaka ya nchi za Ulaya. Wengi kati ya wakimbizi hao ambao wanasumbuliwa na matatizo mengi katika nchi zao kama ukosefu wa amani, umaskini, njaa na matatizo ya kiuchumi, wanaelekea Ulaya kwa matarajio ya kutafuta hali bora ya maisha. Kutokana na hali hiyo mataifa ya Ulaya yamekuwa mbioni kufanya mabadiliko ya sheria za uhamiaji na kuzuia wakimbizi hao kuingia katika nchi za bara hilo.  

Ylva Johansson ambaye ni Kamishna wa Sweden katika Kitengo cha Wakimbizi cha Kamisheni ya Ulaya amesema kumekuwepo changamoto mpya ya wahajiri barani Ulaya katika miezi ya karibuni na kwamba umoja huo unapaswa kuchukua hatu za kujilinda. Ylva Johansson amesema: EU itazidisha idadi ya wanajeshi katika mipaka ya Schengen na kuweka sheria kali za wakimbizi katika nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Kugawana kiadilifu idadi ya wakimbizi baina ya nchi za Ulaya ni moja kati ya masuala yanayozusha mjadala na hitilafu baina ya nchi za bara hilo. Kwa mujibu wa mapatano ya ndani ya Umoja wa Ulaya, nchi nyingi za bara hilo hazilazimiki kuwapokea wakimbizi na zimetoa wito wa kutekelezwa Mkataba wa Dublin. Kwa mujibu wa mkataba huo, wakimbizi wanaoingia barani Ulaya wanapaswa kuomba ukimbizi katika nchi walikoingia kwa mara ya kwanza. Suala hilo linazidisha mashinikizo kwa nchi kama Ugiriki ambazo ziko katika mpaka wa nje wa Ulaya.

Katika upande mwingine hali ya wakimbizi walioko kwenye mipaka ya Ulaya inatajwa kuwa mbaya sana. Idadi kubwa ya wakimbizi hao hufariki dunia kwa kughariki katika Bahari ya Mediterania, wengine hubakia majini wakihangaika kwa njaa na kiu, na baadhi yao wanaobahatika kuwekwa kwenye kambi za wakimbizi wanakabiliana na hali ngumu ya maambukizi ya corona, utumwa wa ngono, magendo ya binadamu na matatizo ya kukosa huduma za afya.

Mkimbizi akijaribu kuingia Ulaya, Libya

Ukweli ni kwamba, nchi za Ulaya ambao zimekuwa zikijigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu zimetupilia mbali nara hiyo na sasa zinatupiana jukumu la kutatua mgogoro huo.

Katika hali hii wakimbizi ndio wahanga wakuu wa hitilafu na migawanyiko hiyo, na inaonekana kuwa, wito wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia wa kufanyika kikao maalumu cha kutafuta suluhisho la mgogoro huo pia hautaweza kupata ufumbuzi wa kadhia hiyo.    

Tags