Aug 13, 2021 09:05 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakosoa vikwazo vya upande mmoja

Wataalamu huru wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wamesema katika taarifa iliyosambazwa Jumatano kwamba vikwazo vya upande mmoja vinavyotekelezwa kimataifa na baadhi ya nchi vimewapokonya watu wengi ulimwenguni haki yao ya kujistawisha kimaendeleo.

Wataalamu hao wamezitaka nchi zinazotekeleza vikwazo vya upande mmoja kukomesha siasa hizo au kwa uchache kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo vinapunguzwa kwa kiasi ambacho hakitadhuru utekelezaji wa sheria au haki za binadamu, zikiwemo za watu kujiendeleza kimaisha. Wataalamu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wamesema katika taarifa hiyo kwamba vikwazo vya upande mmoja ambavyo kwa kawaida hutekelezwa na nchi zenye nguvu na za kibeberu dhidi ya mataifa yanayojitawala duniani huzuia maendeleo ya mataifa huru katika pembe tofauti za duniani na kuwafanya watu wa mataifa hayo kubaki nyuma kimaendeleo.

Ni wazi kuwa wanaolengwa na taarifa hiyo ni Umoja wa Mataifa na mataifa makubwa ya Magharibi na hasa Marekani. Marekani ndiyo nchi kubwa zaidi inayotekeleza vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi nyingine na huwa inatekeleza siasa hizo za vkwazo vya upande mmoja kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu katika pembe tofauti za dunia. Washirika wakuu wa nchi hiyo na hasa Uingerfeza pia wanashirikiana kwa karibu na Marekani katika utekelezaji wa vikwazo hivyo dhidi ya mataifa mengine. Vikwazo vya upande mmoja kwa kawaida hutekelezwa dhidi ya nchi zinazopinga siasa za kibeberu za nchi za Magharibi au zile zinazotuhumiwa kuhatarisha maslahi ya nchi hizo.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran hata katika mazingira ya kuenea virusi vya corona

Marekani bado inatekeleza siasa za vikwazo vya upande mmoja kwa nguvu zake zote hata katika kipindi hiki kigumu ambapo nchi nyingi duniani zinakabiliwa na janga hatari la virusi vya corona. Serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani bado inatekeleza siasa zile zile za mtangulizi wake Donald Trump za kutumia vikwazo vya upande mmoja katika kufikia malengo ya Washington katika nchi tofauti shindani au pinzani ulimwenguni.

Mbali na kutekeleza vikwazo vikali zaidi katika historia yake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia kile kinachotajwa kuwa 'mashinikizo ya juu zaidi', Marekani pia inatekeleza vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi kama Russia, China, Venezuela, Cuba, Syria na Korea Kaskazini. Licha ya Marekani kutekeleza vikwazo hivyo kwa visingizio tofauti vya kisiasa, kibiashara, kiusalama na hata vinahusiana an masuala ya haki za binadamu lakini ni wazi kuwa lengo lake kuu ni kudhamini maslahi yake katika nchi zinazowekewa vikwazo hivyo. Kwa kutilia maanani kwamba vikwazo vya upande mmoja vya Washington dhidi ya mataifa mengine vinatekelezwa bila kibali cha Umoja wa Mataifa ni wazi kuwa vikwazo hivyo vinakiuka sheria za kimataifa.

Umoja wa mataifa umekuwa ukikosoa mara kwa mara vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya nchi nyingine na hasa katika mazingira ya sasa ya kuenea kwa kasi virusi hatari vya corona katika nchi nyingi duniani, na kutaka vikwazo hivyo ama vifutiliwe mbali kabisa au vipunguzwe kwa namna ambayo itaziwezesha nchi zilizo chini ya vikwazo kupata fursa ya kujidhaminia vifaa vya msingi vya afya na matibabu.

Akizungumzia suala hilo, Alena Douhan, mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia uchunguzi wa taathira hasi zinazotokana na hatua za upande mmoja dhidi ya mataifa anasema: Vikwazo vya upande mmoja vinadhoofisha uwezo wa Umoja wa Mataifa, kueneza uoga katika uwanja wa ushirikiano wa kimataifa na utekelezaji sheria.

Alena Douhan

Kwa kutilia maanani taathira hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla dhidi ya mataifa mengine, kuna udharura wa nchi zilizowekewa vikwazo kuunda muungano wa kimataifa kwa lengo la kukabiliana na vikwazo hivyo na hatimaye kuzilazimisha nchi za Magharibi kutazama upya na kurekebisha siasa zao za vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi nyingine. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba wataalamu wa Umoja wa Mataifa tayari wametoa mtazamo wao kuhusiana na matokeo mabaya na hasi ya vikwazo hivyo dhidi ya mataifa huru duniani.

 

Tags