Aug 15, 2021 10:01 UTC
  • Johnson akosoa uamuzi wa Marekani kuhusu Afghanistan

Sambamba na kundi la Taliban kuendelea kuteka maeneo zaidi huko Afghanistan na kuongezeka wasiwasi kuhusu mustakbali wa nchi hiyo, Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza alisema Ijumaa kwamba hali ya Afghanistan ni mbaya mno na kwamba inatokana na uamuzi wa Rais Joe Biden wa kuondoa askari wa Marekani nchini humo.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu zaidi nchini Uingereza ambayo ni mshirika mkuu na wa kistratijia wa Marekani kukosoa waziwazi siasa za Rais Joe Biden wa nchi hiyo kuhusu Afghanistan na kusisitiza kuwa siasa hizo ndizo zimeharibu hali ya nchi hiyo. Kinyume na msimamo wake wa awali wa kubakisha askari wa Marekani Afghanistan, tarehe 8 Julai mwaka huu Biden alitoa amri ya kuondoka mara moja na haraka askari wa nchi hiyo katika ardhi ya Afghanistan na hivyo kuweka wazi mkwamo iliofikia nchini humo. Hali hiyo inashabihiana sana na ile ya kuondoka ghafla askari wa Marekani katika vita huko Vietnam.

Kukwama mazungumzo ya Doha nchini Qatar kati ya kundi la Taliban, Marekani na serikali ya Afghanistan, na wakati huohuo uamuzi wa Washington wa kuondoa ghafla askari wake na wa Nato katika ardhi ya Afghanistan kumetoa fursa kwa Taliban kunufaika na hali hiyo ya vurugu na kuanzisha mashambulizi ya pande zote, ambapo imefanikiwa pakubwa kuteka na hatimaye kudhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan. Hivi sasa kundi hilo linadhibiti zaidi ya asilimia 70 ya ardhi ya nchi hiyo na kuna tetesi kwamba huenda likauteka mji mkuu Kabul muda si mrefu. Baadhi ya vyanzo vya habari vya Afghanistan vinasema kwamba mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje wa Marekani wanamshinikiza Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ajiuzulu.

Taliban wakiendelea kuteka makao makuu ya mikoa ya Afghanistan

Pamoja na hayo, jambo lisilo na shaka katika uwanja huo ni kwamba Biden amekuwa na mchango mkubwa katika matukio yanayoendelea sasa huko Afghanistan. Jeshi la Afghanistan ambalo Marekani inadai kwamba imetumia mabilioni ya dola kuliandaa na kulipa mafunzo yanayohitajika ya kijeshi, limesambaratika kimotisha na kisaikolojia na ndio maana halijachukua hatua yoyote ya maana ya kukabiliana na Taliban bali limeamua kukubali ukweli wa mambo na kujisalimisha mbele ya kundi hilo. Uamuzi wa Biden huko Afghanistan umewatia kiwewe na wasiwasi mkubwa washirika na vibaraka wengine wa nchi hiyo katika eneo kiasi kwamba wameingiwa na shaka iwapo kweli Marekani inaweza kuwadhaminia usalama na msaada wa dharura wakati wa haja.

Kwa hakika Biden ameisaliti serikali ya Afghanistan wakati ambao inahitajia zaidi msaada wake wa kijeshi. Mafanikio makubwa na ya haraka ya kijeshi ya Taliban katika medani ya vita yamepatikana katika hali ambayo washirika muhimu wa Marekani barani Ulaya na Asia walikuwa na matumaini kwamba Biden angehuisha tena nafasi ya Marekani katika ngazi za kimataifa na hasa katika mazingira haya ambapo Russia na China zinatoa ushindani mkali dhidi ya nchi hiyo kwa kuimarisha nafasi zao katika pembe tofauti za dunia. Kurejea nyumba Marekani nchini Afghanistan kumezidisha shaka ya wengi kuhusu misimamo ya nchi hiyo ya Magharibi.

Steven Erlanger, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Kusambaratika haraka Afghanistan kumeibua shaka nyingi kuhusu itibari ya Marekani na kutonesha vidonda vilivyosababishwa na utawala wa Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani. Suala hilo limewafanya wengi waamini kuwa uungaji mkono wa Marekani ni wa kimaslahi tu na ulio na kikomo.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan

Ni wazi kuwa suala hilo halihusiani na Marekani tu bali serikali ya Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza yenyewe pia inalaumiwa katika uwanja huo. Wabunge wengi wa Uingereza walipinga kuondolewa kwa askari wa nchi hiyo huko Afghanistan wakiamini kuwa jambo hilo lingehatarisha usalama wa serikali ya Kabul.

Tags