Aug 20, 2021 00:04 UTC
  • Ripoti mpya kuhusu matokeo ya vita vya miaka 20 vya Marekani huko Afghanistan

Taasisi ya Watson Institute for International and Public Affairs katika Chuo Kikuu cha Brown imetangaza katika ripoti yake mpya kwamba, Marekani imetumia dola trilioni 2.26 katika vita vyake vya miaka 20 huko Afghanistan ambavyo vilianza msimu wa mapukutiko wa mwaka 2001.

Ripoti hiyo inayohitimisha vibaya sana faili la vita na uvamizi wa miongo miwili wa Marekani huko Afghanistan ambako wanajeshi wa nchi hiyo wameondoka kwa njia inayoshabihiana na ile ya kukimbia kwa fedheha wanajeshi wa Marekani huko Saigon nchini Vietnam, inafungua ukurasa mwingine wa kashfa na fedheha ya Washington huko Afghanistan. 

Awali serikali ya Joe Biden ilikuwa imetangaza kuwa, mwenendo wa kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan utakamilika tarehe 11 Septemba 2021. Hata hivyo wanajeshi wa nchi hiyo na nchi nyingine za Magharibi wameondoka mapema zaidi katika ardhi ya Afghanistan. Baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001 katika miji ya New York na Washington, Marekani iliivamia na kuishambulia nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuiondoa madarakani serikali ya kundi la Taliban ambalo inalituhumu kuwa lilishirikiana na al Qaida katika mashambulizi ya Septemba 11. Takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, uharibifu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Katika kipindi hicho wanajeshi 2,448 wa Marekani wameuawa wakiwa vitani, na vilevile wanajeshi 1144 wa shirika la NATO wameuawa katika vita hivyo. wa

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wameuawa Afghanistan

Katika upande mwingine wanajeshi elfu 69 wa Afghanistan, waandishi habari 72 na wafanyakazi 444 wa mashirika ya misaada ya kibinadamu wameuawa katika vita hivyo vya Marekani huko Afghanistan. Takwimu hizi hazijumuishi wale walioaga dunia kutokana na athari mbaya zisizo za moja kwa moja za vita hivyo kama maradhi, ukosefu wa chakula na dawa, uharibifu wa miundombinu na kadhalika.   

Uvamizi wa Marekani na majeshi ya NATO huko Afghanistan umesababisha majanga ya kutisha ikiwa ni pamoja na kuuliwa maelfu ya raia, kuongezeka machafuko na harakati za kigaidi na kustawi kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya. Kufuatia kurejea tena madarakani kundi la Taliban baada ya miaka 20 na kutokana na mapatano ya amani yaliyofikiwa baina ya serikali ya Donald Trump na kundi la Taliban huko Doha nchini Qatar, sasa serikali ya Joe Biden inalazimika kukomesha uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan kwa fedheha, bila ya ghawira na katika hali mbaya zaidi ya ile ya kukimbia wanajeshi wa nchi hiyo huko Vietnam.

Wakati Biden alipoliamuru jeshi la Marekani na lile la NATO kuondoka mara moja na bila ya mpangilio maalumu huko Afghanistan, wataalamu wa mambo na hata maafisa wa serikali ya Kabul walitahadharisha kwamba, jambo hilo yumkini likasababisha ombwe wa kisiasa na kwamba kuna uwezekano makundi kama Taliban yakatumia fursa hiyo kuibua tena vita nchini Afghanistan. Matukio yaliyofuatia ikiwa ni pamoja na kusonga mbele haraka wapiganaji wa Taliban, kusambaratika serikali ya Kabul na hatimaye kutoroka nchi rais Ashraf Ghani baada ya kundi la Taliban kuingia katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, vimesadikisha tahadhari za wataalamu hao.

Kurejea tena madarakani kundi la Taliban huko Afghanistan kunahitimisha miaka 20 ya kile kilichodaiwa na Marekani na waitifaki wake wa Magharibi kuwa ni “kujenga Afghanistan yenye demokrasia ya kisasa”. Mhadhiri wa masuala ya usalama wa kitaifa wa chuo cha vita vya majini cha Marekani, Nikolas Gvosdev anasema: “Kuondoka wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan ni mstari mweusi kwa nchi kama Ukraine, Georgia and Moldova. Tukio hilo limeonesha kwamba, kuwa muitifaki wa Marekani nje ya jumuiya ya NATO hakukua na faida yoyote kwa Afghanistan; bali kinyume chake, hali ya nchi hiyo imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.”

Matokeo ya vita vya Marekani huko Afghanistan yameweka alama kubwa ya kuuliza kuhusu madai ya kupambana na ugaidi ya nchi hiyo yaliyotumiwa na Washington kuivamia Afghanistan hapo mwaka 2001. Itakumbukwa kuwa, katika hotuba yake ya karibuni, Rais Joe Biden alisema lengo la uvamizi wa miaka 20 wa nchi hiyo huko Afghanistan lilikuwa kupambana na ugaidi!

Jenerali Mark Alexander Milley

Sambamba na madai hayo ya Biden, Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Mark Milley pia amehoji sababu na malengo ya nchi hiyo katika vita vyake huko Afghanistan na kusema: Udhibiti wa wapiganaji wa Taliban huko Afghanistan unaweza kuzidisha vitisho vya ugaidi.

Kwa utaratibu huo baada ya uvamizi wa miaka 20, gharama ya trilioni kadhaa za dola na mauaji ya malaki ya watu, Marekani na waitifaki wake wameondoka katika ardhi ya Afghanistan bila ya kupata matunda ya aina yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, ugaidi, dawa za kulevya na uharibifu mkubwa wa nchi hiyo.    

Tags