Aug 25, 2021 12:56 UTC
  • Venezuela yaitaka ICC ichunguze vikwazo vya Marekani dhidi yake

Makamu wa Rais wa Venezuela ameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ifanye uchunguzi juu ya vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini, akisisitiza kuwa vikwazo hivyo ni jinai dhidi ya binadamu.

Delcy Rodriguez ametoa tangazo hilo leo Jumatano katika kikao na waandishi wa habari mjini Caracas na kufafanua kuwa, nchi hiyo ina ushahidi wa kuonesha kuwa vikwazo hivyo vya Marekani vimeathiri haki ya wananchi wa Venezuela ya kupata chakula, matibabu na ustawi wa kiuchumi.

Amesema nchi hiyo imemkabidhi Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC vielelezo vya kuthibitisha madai yake, na kwamba Venezuela ni ya tano katika orodha ya Marekani ya nchi inazozilenga kwa mashinikizo na vikwazo haramu vya upande mmoja.

Maandamano ya kutaka Marekani iache kuingilia mambo ya ndani ya Venezuela

Licha ya kufeli kwa sera za vikwazo za Marekani dhidi ya Venezuela, lakini viongozi wa Washington wangali wamekumbatia siasa hizo za mashinikizo na kuendelea kutekeleza siasa hizo zilizoshindwa na kugonga ukuta dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo amesisitiza mara kadhaa kuwa, nchi yake itaendelea kusimama kidete mkabala wa sera hizo za vikwazo na vita vya kiuchumi vya pande kadhaa.

Tags