Sep 06, 2021 03:00 UTC
  • Onyo la Putin kwa Marekani kwa kuweka mifumo ya makombora katika mpaka wa Russia na Japan

Rais Vladimir Putin wa Russia ameelezea wasiwasi wake kuhusu mpango wa Marekani wa kuweka mifumo yake ya kujilinda kwa makombora katika mpaka wa Russia na Japan na ameitaka Tokyo isiruhusu kufanyika jambo hilo.

Aidha Rais Putin ameitaka Japan itoe uhakikisho wa kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya Tokyo na Moscow. Mgogoro wa visiwa vya Kuril ambavyo vilitekwa na Umoja wa Kisovieti mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia ni kikwazo cha kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya Russia na Japan.

Suala muhimu ambalo Rais Vladimir Putin amelitamka kwa mara ya kwanza ni kwamba iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa baina ya Russia na Japan, basi Marekani italitumia vibaya jambo hilo kwa kuweka mifumo yake ya kujilinda na makombora katika mpaka wa Russia na Japan.

Tangu wakati wa urais wa George W. Bush, ajenda kuu ya Marekani ni kuweka mifumo yake ya kujilinda kwa makombora katika kona zote za kiistratijia duniani, kuanzia barani Ulaya hadi Asia Magharibi na mashariki mwa Asia sambamba na kuweka mifumo hiyo ndani ya ardhi ya Marekani na katika jimbo la Alaska.

Visiwa vya Kuril vyenye mzozo baina ya Russia na Japan

 

Zoezi hilo lilianza kutekelezwa mashariki mwa Asia wakati wa urais wa Barack Obama nchini Marekani na liliendelea pia wakati wa Donald Trump. Mwezi Julai mwaka 2016, Marekani ilifikia makubaliano na Korea Kusini juu ya kuwekwa nchini humo mfumo wa Marekani wa kujilinda na makombora unaoitwa THAAD kwa madai ya kukabiliana na hatari ya Korea Kaskazini. Jambo hilo lilipingwa vikali na Russia na China. Hatua iliyofuatia ilikuwa ni ya mwezi Disemba 2017 ambapo Japan ilitangaza rasmi kuwa imekusudia kutia nguvu uwezo wake wa kujilinda kwa makombora na kwamba imeamua kuweka mifumo miwili ya kujilinda kwa makombora, kutoka nchini Marekani. Kisingizio kilichotumika hapo pia ni hatari ya makombora ya Korea Kaskazini. Mpango huo uliamuliwa kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 2023. Sasa hivi Rais Vladimir Putin wa Russia ameingia wasiwasi kwamba iwapo Moscow na Tokyo zitafikia makubaliano ya amani, basi Marekani itatumia vibaya fursa hiyo kuweka mifumo ya makombora karibu na Russia na kuzidi kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Mara kwa mara Russia imekuwa ikionya kuhusu siasa za Marekani za kueneza mifumo yake ya kujilinda kwa makombora katika maeneo tofauti duniani ikiwemo mashariki mwa Asia. Mara zote Moscow imekuwa ikisema kuwa siasa hizo za Marekani zitakuwa na matokeo mabaya sana kwa usalama wa dunia. Mwanzoni mwa mwaka 2017, Marekani iliweka mfumo wake wa makombora wa THAAD nchini Korea Kusini na sasa hivi inapanua wigo wa siasa zake hizo kwa kushirikiana na Japan.

Mfumo wa makombora wa THAAD

 

Leonid Slutsky, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Russia amesema, kitendo cha Marekani cha kuweka mfumo wake wa makombora wa THAAD mashariki mwa Asia, unaonesha wazi kwamba una malengo mabaya zaidi na si kutokana na madai ya hatari za makombora ya Korea Kaskazini tu.  

Kiujumla Russia inaamini kuwa, kadiri Marekani inavyoongeza mifumo yake ya makombora mashariki mwa Asia ikiwa ni pamoja na karibu mno na Russia, ndivyo Washington inavyojiongezea nguvu za kufanyia ujasusi makombora ya nyuklia na ya kiistratijia ya Russia na China. Moscow inasema kuwa, lengo hasa la Marekani ni kuvunja nguvu kabisa uwezo wa kinyuklia wa Russia na China na matokeo yake kuzidhoofisha kijeshi na kiuchumi nchi hizo mbili ambazo ni wapinzani wa kimataifa wa Marekani. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mara kwa mara viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Russia wakawa wanalalamikia vikali siasa hizo. Zaidi ya hayo ni kuwa, Russia na China zinaamini kwamba, kadiri Marekani inavyowaimarisha kijeshi waitifaki wake kama Japan na Korea Kusini, ndivyo Korea Kaskazini nayo inavyozidi kupata sababu ya kujiimarisha kwa makombora hatari na makubwa zaidi na hilo si kwa manufaa ya usalama wa dunia hata kidogo.

Tags