Sep 09, 2021 07:32 UTC
  • Russia yaionya Israel isiendelee kufanya mashambulio nchini Syria

Mwandishi wa televisheni ya al Mayadeen mjini Moscow amefichua kuwa viongozi wa Russia wamekusudia kutoa onyo kwa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni ili Israel isifanye tena mashambulizi nchini Syria.

Kwa mujibu wa mwandishi wa televisheni hiyo, viongozi wa Russia wamekusudia kutoa onyo kali kwa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni, Yair Lapid, kutokana na utawala huo ghasibu wa kigaidi kuendelea kufanya mashambulizi ya kichokozi dhidi ya Syria. 

Kabla ya hapo Wizara wa Mambo ya Nje wa Syria ilikuwa imetoa tamko ikiutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo kuuzuia utawala wa Kizayuni usiendelee kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Syria vinginevyo umoja huo na baraza lake la usalama ujiandae kubeba jukumu lolote litakalotokea.

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

Mara kwa mara utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Syria ili kuyaunga mkono magenge ya kigaidi. Cha kushangaza ni kuwa si mashirika ya haki za binadamu, si vyombo vya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, vyote vimeshindwa kuchukua hatua za kuilazimisha Israel ikome kufanya mashambulio hayo ndani ya ardhi ya Syria. 

Kwa upande wake Syria imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa, subira yake ina mwisho na siku itakapoamua kulipiza kisasi na kuupiga utawala wa Kizayuni, lawama zote zitakwenda kwa vyombo hivyo hasa Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuzuia uchokozi wa Wazayuni dhidi ya haki ya kujitawala ardhi ya Syria.

Tags