Sep 13, 2021 12:07 UTC
  • Kukiri Biden kushindwa Marekani kukabiliana na al Qaida; kufeli vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi

Rais wa Marekani, Joe Biden, siku ya Jumamosi na pembeni mwa sherehe za mwaka wa 20 wa tangu kutokea mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani, alikiri kwamba yumkini kundi la kigaidi la al Qaida likarejea tena Afghanistan na kusisitiza kuwa, Washington haiwezi kupeleka wanajeshi kila sehemu ilipo al Qaida.

Akijibu swali kwamba je, kundi la al Qaida linaweza kurejea Afghanistan, Biden amesema, ndio na tayari wamerejea katika maeneo mengine duniani. Pamoja na hayo na kwa mara nyingine rais huyo wa Marekani ametetea uamuzi wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan.

Siku chache kabla ya hapo pia, yaani Alkhamisi ya tarehe 9 Septemba 2021, na wakati wa kukaribia kumbukumbu za miaka 20 ya mashambulio ya Septemba 11, Joe Biden alituma ujumbe kwa Baraza la Congress na kutangaza kuongeza muda wa mwaka mmoja, hali ya hatari inayohusiana na vitisho vya kigaidi dhidi ya Marekani ambayo ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001. Hatua hiyo ya kurefusha hali ya hatari kwa muda wa mwaka mmoja inaonesha fikra waliyo nayo wakuu wa kisiasa na kiusalama wa Marekani kuhusu kuendelea vitisho vya kigaidi.

George W. Bush ndiye aliyekuwa rais wa Marekani wakati yalipotokea mashambulio ya Septemba 11. Wakati huo alitangaza vita vya dunia nzima dhidi ya ugaidi na akaamua kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Afghanistan na Iraq. 

Wanamgambo wa al Qaida

 

Zaidi ya watu milioni moja wameuawa katika nchi za Iraq, Afghanistan, Syria, Libya na Yemen katika vita hivyo vilivyodaiwa ni vya kimataifa dhidi ya ugaidi. Sasa hivi miaka 20 imepita tangu yatokee mashambulio ya Septemba 11, ndio kwanza rais wa hivi sasa wa Marekani, Joe Biden anazidi kukiri kuwa si tu wameshindwa kupambana na al Qaida, lakini pia amesema wazi kabisa kuwa Marekani haina uwezo wa kukabiliana na kundi hilo.

Kwa kweli rais huyo wa Marekani anaelewa vyema kwamba, ijapokuwa Washington imetoa pigo kubwa kwa kundi la al Qaida kiasi kwamba wakati wa urais wa Barack Obama, waliweza pia kumuua Osama bin Laden, lakini kundi hilo limeteua mtu wa kushika nafasi ya Osama bin Laden na limekuwa na harakati nyingi katika miaka ya hivi karibuni tena kwenye kona tofauti za dunia hasa Asia Magharibi na barani Afrika.

Jambo hilo linaonesha kushindwa kikamilifu Marekani katika mkakati wa vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi licha ya kuendesha 'stratijia' hiyo kwa muda wa miongo mwili. Mwaka 2001 Marekani iliongoza mashambulizi makubwa dhidi ya Afghanistan. Mwaka 2003 iliivamia Iraq na vile vile kufanya makumi ya operesheni eti za kupambana na ugaidi katika nchi mbalimbali duniani kama vile Yemen, Pakistan na nchi tofauti za Afrika, lakini matokeo yake ni kuwa leo Washington inakiri hadharani kuwa imeshindwa.

Wanajeshi wa Mareekani wakikimbia Afghanistan

 

Daniel Benjamin na Steven Simon kwa pamoja wameandika makala kwenye jarida la Foreign Affairs la Marekani na kusema: Kati ya matokeo mabaya zaidi ya kuanguka serikali ya Afghanistan iliyokuwa inaungwa mkono na Marekani  (ni kupata nguvu makundi ya kigaidi) na hakuna litakalouma zaidi kama kurejea tena al Qaida na makundi mengine ya kigaidi huko Afghanistan. Uvamizi wa kijeshi ambayo ndio njia kuu iliyotumika katika vita vya miongo miwili dhidi ya ugaidi, si tu haukupaswa kufanywa, lakini pia umesababisha madhara makubwa.

Hivi sasa na baada ya kuingia madarakani kundi la Taliban huko Afghanistan, nchi hiyo sasa inahofiwa kuwa maficho mazuri ya makundi mengine ya kigaidi na ya ukufurishaji kama al Qaida na Daesh (ISIS) na ardhi ya nchi hiyo inaweza kutumiwa na makundi hayo kujiimarisha zaidi na kuziathiri pia nchi jirani na za nje ya eneo hili. Hata Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa tahadhari kuhusuu jambo hilo. Rais wa Marekani, Joe Biden naye amekiri kuweko hatari hiyo lakini pamoja na hayo ameshindwa kuonesha njia yoyote ya kutatua mgogoro huo.

Tags