Sep 15, 2021 06:24 UTC
  • Gazeti la Russia: Iran imefelisha njama za Marekani katika Bodi ya Magavana ya IAEA

Gazeti la Kommersant la Russia limeandika kuwa, Iran imefelisha njama za Marekani na waitifaki wake wa Ulaya za kutaka kutoa azimio dhidi ya Tehran katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Gazeti hilo limeripoti kuwa, Marekani na waitifaki wake wa Ulaya walitaka kutumia kikao cha siku ya Jumatatu cha Bodi ya Magavana ya IAEA kupasisha azimio dhidi ya Iran, hata hivyo njama hizo zimefeli hasa baada ya Saeed Khatibzadeh, Msemamji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutangaza kuwa, nchi yake karibuni hivi itaanzisha mazungumzo mjini Vienna kwa ajili ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Saeed Khatibzadeh alisema pia kuwa Tehran haiko tayari kutoa ahadi zozote zile nje ya mapatano ya JCPOA na inasubiri kuona pande nyingine za makubaliano hayo nazo zinaheshimu ahadi zao kivitendo. 

Rafael Grossi (Kulia) katika mazungumzo na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Mohammad Eslami mjini Tehran

 

Gazeti hili limeongeza kuwa, safari ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki alipotembelea Iran siku ya Jumapili, kulitengeneza mambo na kufelisha njama hizo za Marekani na waitifaki wake wa Ulaya ndani ya Bodi ya Magavana ya IAEA.

Jumapili wiki hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zilitoa taarifa ya pamoja na kutilia mkazo suala la kuimarishwa ushirikiano wa kiufundi baina ya pande hizo mbili.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Mohammad Eslami ilisisitizia kuimarishwa ushirikiano wa kiufundi baina ya Iran na wakala huo katika nyanja mbalimbali za masuala ya nishati ya nyuklia. 

Tags