Sep 16, 2021 02:23 UTC
  • Faida kubwa ya mashirika ya kutengeneza silaha ya Marekani kutokana na tukio la Septemba 11

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Watson Institute for International and Public Affairs la Chuo Kikuu cha Brown nchini Marekani, nusu ya bejeti ya wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon baina ya miaka ya 2001 hadi 2020 ambayo inafikia dola trilioni 14 imewaendea wakandarasi na mashirika yanayotenegeneza silaha ya nchi hiyo. Kati ya fedha hizo dola trilioni 4.4 zilitengewa vituo vya kijeshi na viwanda vinavyohusika na masuala ya kijeshi.

Kufuatia tukio la kigaidi la Septemba 11, 2001 huko Marekani, nchi hiyo iliongeza pakubwa bajeti yake ya kijeshi kwa kisingizio cha kuendesha 'vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi' ambapo ilizivamia kijeshi nchi za Afghnaistan na Iraq. Mwaka mmoja baada ya tukio hilo, Marekani iliongeza bajeti yake ya kijeshi kwa asilimia 10. Bajeti hiyo iliongezwa kila mwaka baada ya hapo kwa kadiri kwamba kufikia mwaka huu wa 2021 bajeti hiyo imeongezeka kwa dola bilioni 738.

Miaka 20 baada ya tukio hilo, mashirika makubwa ya kutengeneza silaha ya Marekani yakiwemo ya Lockheed Martin, Boeng, General Dynamics, Raytheon na Northrop Grumman yamejipatia dola trilioni 4.4 kutokana na mikataba iliyosainiwa na Pentagon. Kiwango kikubwa cha faida ya mashirika hayo matano ya Marekani kimeongeza ufisadi nchini humo na pia kiyapelekea kuwa na ushawishi mkubwa katika Congress ya nchi hiyo.

Wakati huo huo wakandarasi wa Marekani na wa nhi nyingine za Magharibi katika kipindi hiki cha miaka 20 wamepata faida nono kutokana na kandarasi walizotengewa katika nchi za Afghanistan na Iraq.

Moja ya silaha zinazotengenezwa na shirika la Lockheed Martin

Marekani inadai kuwa imetumia mabilioni ya dola huko Afghanistan katika miaka 20 iliyopita, pesa ambazo sehemu kubwa haijulikani ilikoenda. Kwa mujibu wa takwimu za karibuni wakandarasi 22,562 wamekuwa wakijishughulisha na mambo tofauti huko Afghanistan.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Machi mwaka huu na John Sopko, Inspekta Mkuu Maalumu kwa ajili ya Ukarabati wa Afghanistan, Marekani ilitumia mabilioni ya dola kwa ajili ya majengo na magari ambayo baadaye yalitumiwa vibaya au hayakutumika kabisa. Katika ripoti zake za miaka ya kabla ya hapo, Sopko alisema kwamba taasisi na wizara za Marekani na hasa Pentagon na Wizara ya Mambo ya Nje zilihusika na ubadhirifu, ufisadi na wizi mkubwa wa fedha za umma za walipakodi wa Marekani zilizotengewa Afghanistan. Mwaka 2011 kemisheni maalumu iliyobuniwa kwa ajili ya kuchunguza kandarasi zilizotiwa saini katika kipindi cha vita vya Afganistan na Iraq iliripoti kuhusu hongo, ubadhirifu na wizi mkubwa wa fedha uliofanyika katika nchi hizo wa dola bilioni 60.

Shirika la Watson Institute for International and Public Affairs pia katikati ya mwezi Agosti uliopita lilichapisha ripoti iliyosema kwamba uvamizi wa Marekani uliomalizika rasmi tarehe 31 Agosti mwaka huu umeigharimu Marekani dola trilioni 2.26.

Kipindi cha Marekani kufanya kampeni ya kimataifa kwa ajili ya kuivamia Afghanistan na Iraq kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, kilichukuliwa na mashirika ya kutengeneza silaha ya Marekani kuwa fursa nzuri na ya kipekee kwa ajili ya kufunga mikataba ya kuiuzia Pentagon silaha mpya ambazo zingetumika katika nchi hizo zilizovamiwa kijeshi na Marekani. Mikataba hiyo hatimaye iliyapelekea mashirika hayo ya utengenezaji silaha kupata faida kubwa ya mabilioni ya dola.

Askari vamizi wa Marekani nchini Afghanistan

Nukta ya kuzingatia hapa ni kuwa Marekani ambayo inadai kumalizika rasmi uvamizi wake wa kijeshi huko Afghanistan na ambapo sasa inajiandaa kuondoa askari wake katika ardhi ya Iraq, badala ya kupunguza bejeti yake ya kijeshi na kuitumia katika miradi ya maendeleo kwa maslahi ya Wamarekani, imeongeza bajeti hiyo katika matumizi ya mwaka ujao wa 2022, ambapo faida ya miwsho itayaendea mashirika na viwanda vya kijeshi vya nchi hiyo.

Ro Khanna, mbunge wa chama cha Democrat cha Marekani anasema: Tunapasa kufanya mabadiliko ya msingi kuhusu namna ya kugharamia masuala ya usalama wa taifa, uwekezaji katika masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi na kushughulikia suala la maambukizi ya corona. Haya ndiyo mambo yanayodhamini zaidi usalama wa Wamarekani kuliko gharama kubwa ya mabilioni ya dola zinazotumika kwa ajili ya kununua silaha.

Tags