Sep 16, 2021 02:24 UTC
  • Mbunge Muislamu wa Uingereza alipua kombora bungeni, aeleza jinsi anavyosumbuliwa na Islamophobia

Mbunge mwanamke wa Kiislamu katika Bunge la Uingereza amezusha mjadala mkubwa ndani ya bunge la nchi hiyo baada ya kufichua manyanyaso na ubaguzi wanaokabiliana nao kila siku wanawake wa Kiislamu nchini Uingereza.

Matamshi makali ya Zarah Sultana yametolewa wakati mashinikizo yakiongezeka dhidi ya serikali ya Uingereza yakiitaka kuarifisha rasmi "Islamophobia" baada ya mjadala huo kucheleweshwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Zarah Sultana amelisomea Bunge la Uingereza ujumbe na barua anazoandikiwa zilizojaa matus, maneno ya ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu ambazo zimelitikisa na kulishtua bunge na wanasiasa wengi wa nchi hiyo

Mbunge Zarah Sultana ambaye ameshindwa kuzuia machozi yake wakati nahutubia kikao cha Bunge amesimulia hali ya wahka na wasiwasi anayoishi nayo tangu alipojitokeza kugombea nafasi hiyo katika eneobunge la Coventry South huku akishuhudia jinsi Waslamu waliofanukiwa kupata vyeo nchini Uingereza wanavyokabiliana na hujuma na chuki za kidini tangu waliposhika nyadhifa hizo.

Zarah Sultana ameashiria baadhi jumbe alizutumiwa na wabaguzi dhidi ya Waislamu nchini Uingereza baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kama zile zinazosema: "Wewe na Waislamu wenzako ni hatari halisi kwa wanadamu", "wewe ni saratani popote pale unapokuwa, na Ulaya itakutema hivi karibuni", na ujumbe mwingine uliosema: wewe ni taka katika dunia hii na hapana budi kuusafisha ulimwengu na kuondoa takataka hizo".

Zarah Sultana

Saltana ambaye alikuwa akizungumza kwa maumivu makubwa amesema, awali alidhani kwamba hali ya hujuma na chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza itaboreka lakini ukweli ni kinyume chake, kwa sababu "Islamophobia na chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza ni hakika ambayo haiwezekani kuificha."

Mbunge huyo wa Uingereza ametahadharisha kuwa, kunyamazia kimya ubaguzi dhidi ya Waislamu kunawashajiisha zaidi wabaguzi na kuwafanya wazidishe hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu, watu weusi, wakimbizi, Mayahudi na kadhalika.

Zarah Sultana pia ameashiria matamshi yaliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza, Boris Johnson akiwataja wanawake wanaovaa nikabu kuwa ni sawa na "masanduku ya posta au wezi wa mabenki", na kusema matamshi kama haya yanachochea zaidi ubaguzi.

Matamshi hayo ya mbunge Zarah Sultana yamepokewa kwa wingi katika mitandao ya kijamii ya hotuba yake imeangaliwa na zaidi ya watu nusu milioni katika kipindi cha chini ya siku mbili.