Sep 16, 2021 02:24 UTC
  • WHO: Watu wasiopungua 137,000 huaga dunia kila mwaka kwa kuumwa na nyoka

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, watu 81,000 hadi 137,000 hupoteza maisha kila mwaka katika maeneo mbalimbali duniani kutokana na athari zinazosababishwa na kuumwa na nyoka wenye sumu.

Tangazo hilo limetolewa katika hafla ya uzinduzi wa  jukwaa maalum mtandaoni kwa lengo la kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu hatari ya kuumwa na nyoka wenye sumu na wapi waliko nyoka hao hatari zaidi duniani.

Aidha taarifa hiyo imeelezwa kwamba, mbali ya vifo vya watu hadi 137,000 kila mwaka, kuumwa na nyoka pia kumewaacha mamilioni ya watu na vilema vya maisha.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema, kuumwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa ambayo inapelekea ulemavu wa maisha na kukatwa viungo.

 

Waathirika wakubwa ni watu wanaofanyakazi katika sekta ya kilimo na watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hasa katika maeneo ya vijijini.

Kwa mfano barani Asia watu wapatao milioni 2 hudhurika na sumu ya nyoka kila mwaka na Afrika watu 435,000 hadi 580,000 huhitaji matibabu kila mwaka baada ya kuumwa na nyoka.

Kwa mujibu wa WHO ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kuumwa na nyoka, kwanza  ni lazima kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, pili kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, tatu kuimarisha mifumo ya afya na nne kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hii.