Sep 16, 2021 07:51 UTC
  • Ulimwengu umefumbia macho silaha za nyuklia za Israel kwa zaidi ya miongo mitano

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekosoa vikali kimya cha makusudi cha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuhusu urundikaji wa silaha hatari za nyuklia unaofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel. Imesema kimya hicho kimekuwa kikiendelea kwa zaidi ya miongo mitano sasa.

Akifafanua suala hilo, Kazem Gharibabadi, balozi wa Iran katika mashirika ya kimataifa yaliyo na makao makuu yao huko Vienna Austria alisema jana Jumatano katika hutuba yake kwa bodi ya magavana ya IAEA kwamba, jamii ya kimataifa na wakala huo wa kimataifa zimefumbia macho ukweli huo mchungu na kutochukua hatua yoyote kwa ajili ya kukagua maghala ya utawala wa Kizayuni ya silaha hizo, wala vituo vyake vya kutengeneza silaha za atomiki na kemikali.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ametoa matasmhi hayo kufuatia tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa karibuni na mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na Marekani, Gilad Erdan kwamba IAEA imefumbia macho shughuli za nyuklia za Iran kwa miezi saba iliyopita.

Silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni

Mwezi Februari, Iran ilisimamisha kwa muda utekelezaji wa protokali ziada ya IAEA iliyoruhusu wakaguzi wa wakala huo kuweza kufanya ukaguzi wa ghafla na usiotangazwa mapema katika vituo vya nyuklia vya Iran. Hatua hiyo ya Iran ilitokana na uamuazi wa nchi nyingine zilizotia saini mkataba wa nyuklia mwaka 2015 wa kutotekeleza majukumu yao katika mkataba huo. Pamoja na hayo bado lakini wakala wa IAEA unaruhusiwa kufanya ukaguzi mwingine wa kawaida katika vituo hivyo.

 Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekataa katakata kuruhusu wakaguzi wa IAEA kufanya uchunguzi na ukaguzi katika vituo na viwanda vyake vya nyuklia umekataa kutia saini mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia NPT, ambapo unakisiwa kujirundikia vichwa vya nyuklia kati ya 200 hadi 400 katika maghala yake ya silaha za mauaji ya umati.