Sep 16, 2021 12:17 UTC
  • UNICEF yataka shule zilizofungwa kwa corona zifunguliwe kote ulimwenguni

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limezitaka mamlaka zinazohusika na elimu katika kona zote za dunia zihakikishe kuwa zinafungua haraka shule zilizokuwa zimefungwa kutokana na UVIKO-19.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Reuters ambalo limesema kwamba, takwimu za UNICEF zinaonesha kuwa, shule zimefungwa kikamilifu katika nchi 17 duniani na katika nchi 39 shule hizo zimefunguliwa nusu tu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ufilipino, Bangladesh, Venezuela, Saudi Arabia na Panama ni miongoni mwa nchi ambazo shule zao nyingi zimefungwa kutokana na ugonjwa wa corona au UVIKO-19. Sasa hivi karibu watoto milioni 77 wameshindwa kwenda shule katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, kwenye nchi hizo.

Skuli nyingi zimefungwa duniani kutokana na UVIKO-19

 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amesisitiza kuwa, mgogoro wa kutoa elimu duniani bado unaendelea na kila siku ambayo shule inafungwa huwa ni hasara kubwa.

Ripoti hiyo ya UNICEF imeongeza kuwa, kati ya wanafunzi na walimu, walimu ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele katika kupigwa chanjo za kujikinga na corona. Vile vile katika jamii, walimu wanapaswa wapewe vipaumbele vya awali katika zoezi la kutoa chanjo za UVIKO-19.

Kwa mujibu wa tovuti ya worldmeters inayotoa takwimu mubashara za ugonjwa wa corona, hadi leo mchana watu milioni 227 na 334,700 walikuwa wameshaambukizwa ugonjwa huo kote duniani. Kati ya hao, 4,675,053 walikuwa wameshafariki dunia na milioini 204 na 29,104 walikuwa wameshapata afueni na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Tags