Sep 17, 2021 02:39 UTC
  • Russia yakosa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu haki za wanawake

Naibu mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa mjini New York amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kwamba nchi za Magharibi zinatumia vigezo vya kindumakuwili kuhusu haki za wanawake huko Afghanistan na katika eneo la Idlib nchini Syria.

Dmitry Chumakov amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi za Magharibi zinaeleza wasiwasi wao kuhusu haki za wanawake wa Afghanistan na wakati huo huo zinafumbia macho hali mbaya ya haki za wanawake na wasichana katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi hizo huko Syria.

Mwanadiplomasia huyo wa Russia amekumbusha kwamba, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alikuwa tayari ametahadharisha kuhusiana na suala hilo na kusema kuwa, raia wakiwemo wanawake na watoto wanaoishi katika maeneo ya mkoa wa Idlib yanayodhibitiwa na makundi ya kigaidi nchini Syria, wanateswa na kunyanyaswa.

Idlib, Syria

Dmitry Chumakov amesema Russia ina wasiwasi kwamba misaada ya kibinadamu iliyotumwa huko Syria yumkini imeporwa au kuuzwa, na kwamba hakuna utaratibu maalumu wa kusambaza misaada hiyo kwa njia ya uadilifu. Amesisitiza kuwa misaada hiyo haikufikishwa kwa wananchi wanaohitajia wa Syria na badala yake inahifadhiwa katika maghala ya watu wasiojulikana ambao nchi za Magharibi zinawataja eti "washirika wa kuaminika".  

Tags