Sep 17, 2021 07:27 UTC
  • Nusu ya wanunuzi wa silaha nchini Marekani ni wanawake

Matokeo ya utafiti mpya uliofanywa nchini Marekani yanaonyesha kuwa tangu mwaka 2019 hadi mwezi Aprili mwaka huu wanawake wameunda karibu ya nusu ya wamiliki wapya wa silaha nchini humo.

Uchunguzi uliofanywa kitaifa kuhusu hali ya umiliki wa silaha moto katika mwaka huu wa 2021 na wataalamu wa kitivo cha afya ya jamii katika chuo kikuu cha Harvard unaonyesha kuwa, kuanzia Januari 2019 hadi Aprili mwaka huu, wanawake wapatao milioni 5.3 wa Kimarekani wamenunua silaha kwa mara ya kwanza.

Karibu wanaume milioni nne wa nchi hiyo, nao pia walinunua silaha katika kipindi hicho.

Chunguzi zilizowahi kufanywa katika miongo kadhaa nyuma nchini Marekani zilionyesha kuwa, soko la silaha moto la nchi hiyo lilikuwa na asilimia 10 hadi 20 tu ya washitiri wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Dk. Deborah Azrael, mtafiti wa kitivo hicho afya ya jamii katika chuo kikuu cha Harvard, katika utafiti wao, walichunguza rekodi za watu 19,000 na kwamba huo ulikuwa utafiti mpana na jumuishi zaidi kitaifa kufanywa nchini Marekani kuhusiana na ununuzi wa silaha.

Duka la silaha Marekani

Watafiti wanasema, sababu ya kuongezeka idadi ya wanawake wanaonunua silaha nchini Marekani ni janga la dunia nzima la maradhi ya Covid-19, malalamiko ya kijamii, yakiwemo yale yaliyogubikwa na machafuko kufuatia mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd yaliyofanywa na askari polisi wa jimbo la Minnesota, na vilevile machafuko ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo wa mwaka 2020.

Uchunguzi huo umeonyesha pia kuwa, asilimia 55 ya wanunuzi wapya wa silaha nchini Marekani ni wazungu, asilimia 21 ni Wamarekani weusi na asilimia 19 ni wale wenye asili ya Latini. Kwa upande wa wanunuzi wanawake, Wamarekani weusi wanaunda asilimia 28 tu ya wanunuzi hao wa silaha moto.../

Tags