Sep 19, 2021 02:22 UTC
  • Kushadidi mivutano baina ya Marekani na Ufaransa, Paris yamwita nyumbani balozi wake mjini Washington

Ufaransa imechukua uamuzi wa kumwita nyumbani balozi wake mjini Washington sambamba na kushadidi mivutano katika uhusiano wa serikali ya Paris na Marekani. Vilevile imechukua hatua ya kumrejesha nyumbani balozi wake nchini Australia kama hatua ya kuonesha malalamiko yake.

Alkhamisi iliyopita serikali ya Ufaransa ilitangaza waziwazi kutoridhishwa na tangazo la kuanzishwa muungano wa pande tatu za Marekani, Uingereza na Australia ambao umepelekea kufutwa mkataba wa mauzo ya silaha wenye thamani ya dola bilioni 90 baina kampuni moja ya Ufaransa na serikali ya Australia kwa ajili ya kuunda nyambizi. 

Baada ya kutiwa saini makubaliano hayo ya ushirikiano wa pande tatu, Paris ilifuta sherehe iliyokuwa imepangwa kufanyika Ijumaa iliyopita katika ubalozi wake mjini Washington kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 240 wa vita vya Chesapeake (Battle of the Chesapeake).

Afisa mmoja wa Ufaransa amesema kuwa, kufanyika sherehe hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuimarisha muungano wa Marekani na Ufaransa kungekuwa "kichekesho" baada ya kutangazwa muungano mpya wa pande hizo tatu. Mkabala wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken anafanya jitihada za kutuliza hali ya mambo akidai kuwa, Washington inaupa thamani makhsusi uhusiano na ushirikiano wake na Ufaransa.

Inaonekana kuwa uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantic umeingia katika awamu mpya ya ghasia na mivutano. Tangu alipoingia White House, Rais Joe Biden wa Marekani amekuwa akiashiria mpasuko na hali isiyofaa ya uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantic iliyosababishwa na siasa za mtangulizi wake, Donald Trump na kuahidi kufanya mageuzi katika uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuanzisha tena ushirikiano baina ya Ulaya na Marekani. 

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump 

Hata hivyo imebainika kuwa, matamshi hayo ya Biden na Blinken ni nara tupu, kwa sababu katika matendo na nyendo zake, Washington imeendeleza sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kujali maslahi yake binafsi bila ya kutilia maanani washirika wake wa Ulaya.   

Kielelezo cha wazi cha ukweli huo ni utendaji wa Biden huko Aghanistan ambako kiongozi huyo mepuuza mitazamo ya wanachama wa Ulaya katika jumuiya ya NATO kuhusiana na suala la kuondoa wanajeshi wa nchi za Magharibi huko Afghanistan. Nchi za Ulaya zinaamini kuwa, tajiriba ya Afghanistan imeonesha kuwa, tangu sasa kuna ulazima wa kuwa na tahadhari katika kuifuata Marekani kwenye masuala ya kikanda na kimataifa.  

Kwa sasa Marekani imetoa pigo jingine kwa nchi kubwa ya pili kwa umuhimu zaidi ya Ulaya yaani Ufaransa katika fremu ileile ya sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kupuuza maslahi ya pande nyingine.

Baada ya kuanzisha muungano huo mpya na waitifaki wake wa siku nyingi yaani Uingereza na Australia katika masuala yanayohusiana na eneo la Indo-Pacific uliopewa jina la AUKUS, Marekani pia imetangaza kuwa itaipatia Australia teknolojia ya kuunda nyambizi za nyuklia. Hatua hii ya Marekani ya kumpa mmoja kati ya waitifaki wake teknolojia nyeti kama hiyo ina ishara yenye kutoa maana maalumu. Mwaka 1958 Marekani iliipatia Uingereza teknolojia ya kuunda nyambizi za nyuklia. Suala hili linaonesha umuhimu mkubwa wa Australia katika stratijia ya kijeshi na kiusalama ya Marekani katika eneo la Indo-Pacific. Kwa hakika Marekani inakusudia kuimarisha zaidi jeshi la Australia kwa shabaha ya kukabiliana na harakati za China katika eneo hilo.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Reza Ishawi anasema: “Katika hatua ya kukabiliana na China, Marekani na Uingereza zinafanya jitihada za kuifanya Australia askari wa mstari wa mbele katika makabiliano ya kijeshi na China.” Pamoja na hayo hatua hiyo imeitoa pigo kubwa kwa nchi za Ulaya hususan Ufaransa. Kuvunjwa mkataba wenye thamani ya dola bilioni 90 baina ya Ufaransa na Australia kwa ajili ya kuunda nyambizi 12 kumeitia hasara kubwa sana za kiuchumi Ufaransa na kutoa pigo kwa hadhi ya nchi hiyo.

Ukweli ni kwamba, kwa kutilia maanani matamshi yaliyotolewa na Biden kuhusu uhusiano mkubwa wa Paris na Washington, Wafaransa hawakutarajia hata kidoto kuzabwa kibao kikali kama hicho na serikali ya Marekani inayodai kuimarisha ushirikiano wa pande mbili za Babari ya Atlantic.

Rais wa Marekani, Je Biden 

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, akaitaja hatua hiyo ya Marekani kuwa ni usaliti na kudungwa jambia mgongoni na kwamba inakumbusha mienendo ya Donald Trump.

Tags