Sep 19, 2021 07:16 UTC
  • Washington: Kwa sasa Russia ni tishio kubwa zaidi kwa Marekani kuliko China

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani amedai kwamba kwa sasa Russia ni tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo na Ulaya kuliko China.

Colin Kahl ambaye alikuwa akizungumza karibuni katika kikao cha masuala ya kijeshi cha eneo la Baltic huko Lithuania amesema kwamba katika miaka michache ijayo, huenda Russia ikadhihiri kuwa changamoto kubwa ya kiusalama na kijeshi kwa Marekani na bara zima la Ulaya. Amedai kuwa Russia ni adui mkubwa kwa Marekani na Uyala na ambaye amekuwa na athari hasi na haribifu katika ngazi za kimataifa.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani ameongeza kuwa pamoja na kuwa China huenda ikawa tishio kubwa kwa Washington na washirika wake katika kipindi kirefu lakini Russia ni changamoto kubwa zaidi kwa pande hizo katika kipindi kifupi, jambo ambalo linaoonekana wazi katika siasa na nyenendo za nchi hiyo barani Ulaya, Asia, Asia Magharibi na katika mitandao ya intaneti.

Wanajeshi wa Marekani katika gwaride nchini Lithuania

Colin Kahl amesisitiza kwamba Marekani inafuatilia kwa karibu mienendo na harakati za kijeshi za Russia katika mipaka ya mashriki ya nchi wanachama wa shirika la kijeshi la Nato na katika eneo la Bahari Nyeusi.

Afisa huyo wa kijeshi wa Marekani wakati huo huo amedai kwamba Marekani iko tayari kufanya mazungumzo na Russia iwapo viongozi wa Moscow watabadilisha sera zao za kijeshi.

Kikao cha kijeshi cha Baltic huandaliwa kila mwaka na Wizara ya Ulinzi ya Lithuania kwa ajili ya kuchunguza na kijadili masuala ya kiusalama na kijeshi.

Tags