Sep 19, 2021 16:33 UTC
  • Familia ya Waafghani waliouawa na Marekani: Kuungama hakutoshi, wahusika wachukuliwe hatua

Familia ya raia kumi wa Afghanistan waliouawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani mjini Kabul imekataa hatua ya serikali ya Washington ya kuungama na kuomba radhi kutokana mauajii hayo.

Familia hiyo imesema kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuomba radhi kwa kuua ndugu na watoto wao haitoshi na kwamba hujuma hiyo ni jinai ya kivita. Familia hiyo imetoa wito wa kuchukuliwa hatua maafisa waliohusika na mauaji hayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Tarehe 29 mwezi Agosti mwaka huu ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani ilishambulia gari na eneo la raia mjini Kabul na baadaye Marekani ilidai kuwa imezima jaribio la shambulizi ya kujilipua kwa mabomu la tawi la kundi la kigaidi la Daesh. Hata hivyo familia ya dereva Aimal Ahmadi aliyeuawa katika shambulizi hilo ilisema alikuwa akifanya kazi kwenye asasi isiyo ya serikali, na kwamba watu 10 waliuawa katika hujuma hiyo ya jeshi la Marekani.

Siku ya Ijumaa, kamanda wa vikosi vya kigaidi vya Marekani katika eneo la asia Magharibi CENTCOM, Jenerali Frank McKenzie alitangaza mjini Wshington katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon kwamba, uchunguzi wa kijeshi kuhusu shambulio la anga la tarehe 29 Agosti lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya nchi hiyo mjini Kabul umeonyesha kuwa, raia 10 wakiwemo watoto saba waliuawa katika shambulio hilo; na kuna uwezekano dereva na gari lililolengwa katika shambulio hilo halikuwa tishio wala halikuwa la kundi la kigaidi la DAESH.

Jenerali Frank McKenzie

Wakati huo huo Shirika la Msamaha Duniani limeeleza katika taarifa kwamba, linakaribisha ungamo la Marekani kwamba iliua raia katika shambulio la anga la tarehe 29 Agosti mjini Kabul na limeitaka Washington ikiri pia kuhusu jinai ilizotenda katika nchi zingine duniani.

Tags