Sep 20, 2021 03:01 UTC
  • Bernie Sanders
    Bernie Sanders

Mwanasiasa, mwanaharakati na seneta mashuhuri wa jimbo la Vermont nchini Marekani amesema kuwa shambulizi lililofanywa na jeshi la nchi hiyo huko Afghanistan ambalo limeua raia 10 wasio na hatia yoyote ni maafa ya binadamu.

Bernie Sanders amesema anatarajia kuwa viongozi wa White House wameelewa ukubwa wa maafa yaliyofanyika na watahakikisha kwamba jambo kama hilo halikaririwi. 

Mwezi mmoja baada ya shambulizi hilo lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani mjini Kabul na kuua raia wasio na hatia, kamanda wa vikosi vya kigaidi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi CENTCOM, Jenerali Frank McKenzie alitangaza Ijumaa iliiyopita mjini Washington kwamba, uchunguzi wa kijeshi kuhusu shambulio la anga la tarehe 29 Agosti lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya nchi hiyo mjini Kabul umeonyesha kuwa, raia 10 wakiwemo watoto saba waliuawa katika shambulio hilo. Jenerali McKenzie alisema, kuna uwezekano dereva na gari lililolengwa katika shambulio hilo halikuwa tishio wala halikuwa la kundi la kigaidi la DAESH. 

Raia wasiopungua 10 wa Afghanistan waliuawa katika shambulizi la Marekani mjini Kabul

Kamanda wa majeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi CENTCOM, alikiri kufanya makosa na kusema yeye mwenyewe anakubali kubeba dhima ya yaliyotokea. 

Hata hivyo familia ya raia kumi wa Afghanistan waliouawa katika shambulizi hilo imesema kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuomba radhi kwa kuua ndugu na watoto wao haitoshi na kwamba hujuma hiyo ni jinai ya kivita. Familia hiyo imetoa wito wa kuchukuliwa hatua maafisa waliohusika na mauaji hayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Tags