Sep 20, 2021 10:14 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN awataka viongozi wa dunia 'waamke' wabadili muelekeo na waungane

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa viongozi duniani ‘waamke’ wabadili mwelekeo, wachukue mwelekeo sahihi katika nchi zao na duniani na waungane.

Guterres ametoa mwito huo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa kwa mnasaba wa kuwadia mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika mahojiano hayo, Katibu Mkuu wa UN amezungumzia hali halisi ya taasisi za umoja huo kwa kusema: "Taasisi tulizo nazo hazina meno. Na wakati mwingine hata pale ambapo zina meno kama ilivyo kwa Baraza la Usalama, hazina hamu ya kutafuna."

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo ambayo amefanyiwa na shirika la habari la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amegusia pia janga la dunia nzima la maradhi ya Covid-19 na hasa suala la chanjo ya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona na akasisitiza kuwepo kwa mpango sawia wa kimataifa katika utoaji chanjo, wakati huu ambapo aina tofauti tofauti za virusi vya corona zinaendelea kuripotiwa; aina ambazo zinaweza kuwa sugu kwa chanjo iliyopo hivi sasa.

Ukumbi wa mkutano wa Baraza Kuu la UN

Kuhusu Afghanistan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, hali ya huko haitabiriki na akaongeza kwamba: "Kile kilichotokea Afghanistan kinaweza kuwa kivutio kwa makundi ya kigaidi au harakati nyingine za waasi kuimarika zaidi."

António Guterres amezungumzia pia suala la mabadiliko ya tabianchi na akatoa indhari kwa kusema: "dunia iko katika hatari ya kutumbukia kwenye korongo”.

Aidha ametoa mwito kwa nchi wanachama kuhakikisha mkutano ujao wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 unakuwa wa mafanikio.

Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika ngazi ya viongozi wa juu wa mataifa wanachama unatazamiwa kuanza rasmi kesho Jumanne tarehe 21 Septemba.../