Sep 20, 2021 10:48 UTC
  • Makumi wauawa na kujeruhiwa katika ufyatuaji risasi uliotokea kwenye chuo kikuu, Russia

Watu wasiopungua wanane wameuawa na wengine wasiopungua 19 wamejeruhiwa baada ya mwanachuo aliyekuwa na silaha kufyatua risasi ndani ya jengo la chuo kikuu cha mji wa Perm ulioko umbali wa kilomita 1,800 mashariki ya mji mkuu wa Russia, Moscow.

Vyombo vya habari kutoka mjini Perm vimeripoti kuwa, mshambuliaji huyo alikamatwa mara baada ya hujuma hiyo aliyofanya katika chuo kikuu hicho cha serikali leo asubuhi.

Vyombo vya habari vya Russia vimeonyesha taswira za wanachuo waliokuwa wakipiga mbio kunusuru maisha yao, huku baadhi yao wakichupa kutokea kwenye madirisha ya ghorofa ya kwanza ya jengo la chuo na kuanguka chini kwa kishindo kabla ya kutimua mbio tena kwa ajili ya usalama wao.

Semyon Kasryakin, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Perm amevieleza vyombo ya habari kuwa, walilazimika kujifungia darasani na kuweka kizuizi mlangoni kwa kutumia viti ili kumzuia mshambuliaji huyo asiweze kuingia ndani ya darasa hilo lililokuwa limehifadhi watu wapatao 60.

Kwa mujibu wa duru za hospitali, baadhi ya majeruhi waliumia kwa majeraha ya risasi na wengine waliumia wakati walipokuwa wakikimbia kunusuru maisha yao.

Wanafunzi wakichupa madirishani kunusuru maishani

Matukio ya ufyatuaji risasi hutokea kwa nadra sana katika skuli na vyuo vikuu nchini Russia.

Mnamo tarehe 11 Mei mwaka huu, kijana barobaro aliwafyatulia risasi na kuwaua wanafunzi saba wa shule na walimu wawili katika eneo la Kazan na kupelekea Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo kutoa agizo la kuwekwa masharti makali zaidi ya umiliki silaha.

Russia ina sheria kali za umiliki wa silaha moto kwa raia, lakini baadhi ya aina za silaha huweza kupatikana kwa ajili ya uwindaji, kujilinda au michezo, baada ya mwombaji kukidhi masharti na majaribio anayofanyiwa.../

Tags