Sep 21, 2021 02:39 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Mataifa juu ya kukiuka sheria vikwazo vya upande mmoja vya Marekani

Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu taathira hasi za vikwazo vya upande mmoja dhidi ya haki za binadamu amesisitiza kwamba vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinakiuka wazi sheria za kimataifa.

Akizungumza karibuni katika Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Matifa, Alena Douhan ametaka vikwazo hivyo vifutiliwe mbali mara moja na wakati huo huo kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa libuni mchakato utakaopunguza taathira hasi za vikwazo hivyo. Douhan ameashiria sheria ya Caesar ambayo ilipasishwa na Congress ya Marekani mwaka 2019 dhidi ya Syria na kusema sheria hiyo ni mfano wa wazi wa kutekelezwa sheria za ndani ya nchi moja nje ya mipaka yake.

Sheria hiyo ilianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka 2020. Kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo inalenga kutoa mashinikizo dhidi ya Syria, mashirika, taasisi na raia wa nchi hiyo wanaweza kuwekewa vikwazo na Marekani kwa ajili ya kuwashinikiza wasalimu amri mbele ya matakwa ya Washington.

Alena Douhan

Marekani ndio nchi kubwa zaidi duniani inayotekeleza mashinikizo na vikwazo dhidi ya mataifa mengine kwa lengo la kuyalazimisha yatii na kutekeleza siasa zake za nje. Washirika wa nchi hiyo pia wanashirikiana nayo katika uwanja huo kama tunavyoona Umoja wa Ulaya ukitekeleza vikwazo hivyo dhidi ya Syria.

Hata kama Rais Joe Biden wa Marekani anadai kufanya mabadiliko katika siasa za nje za nchi hiyo lakini ni wazi kuwa bado anafuata siasa zile zile za mtangulizi wake Donald Trump za kutumia vikwazo dhidi ya mataifa pinzani na shindani kama wenzo wa kudhamini maslahi ya Washington nje ya mipaka yake.

Kwa kutilia maanani kwamba vikwazo vingi vya Marekani vinatekelezwa kwa upande mmoja na bila kuwa na kibali cha Umoja wa Mataifa, ni wazi kuwa vikwazo hivyo vinakiuka sheria za kimataifa. Mbali na kutekeleza vikwazo vikali zaidi katika historia yake dhidi ya taifa la Iran kupitia siasa za mashinikizo ya juu kabisa, Marekani pia inatekeleza siasa za vikwazo dhidi ya nchi nyingine kama Russia, China, Syria, Venezuela, Cuba na Korea Kaskazini.

Licha ya vikwazo hivyo kutekelezwa kwa visingizio mbalimbali vya kisiasa, kibiashara, kiusama na hata kwa madai yasiyo na msingi kuhusu haki za binadamu, lakini la muhimu ni kuwa vinatekelezwa kwa madhumuni ya kudhamini maslahi ya Marekani. Kwa mujibu wa, Alexander Novak, waziri wa nishati wa Russia, ulimwengu umechoshwa na vikwazo hivyo vya Marekani ambavyo havizingatii sheria yoyote ya kimataifa wala kutelelezwa kwa idhini ya Umoja wa Mataifa.

Ni wazi kuwa Umoja wa Mataifa imekosoa mara nyingi vikwazo hivyo vya upande mmoja vya Marekani na hasa katika kipindi hiki cha kuenea duniani virusi hatari vya corona, na kutaka viondolewe mara moja ili kuruhusu nchi zilizowekewa vikwazo zipate njia za kufikia kirahisi madawa na bidhaa za kitiba kwa ajili ya kupambana na maradhi hayo. Alena Douhan anaamini kuwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinadhoofisha nafasi ya Umoja wa Maaifa katika kutekeleza majukumu yake ya kimataifa, kuzitia hofu nchi nyingine na kuzifanya zisishirikiane inavyotakikana na mataifa mengine na wakati huo huo kukanyaga sheria za kimataifa.

Marekani na washirika wake zinatumia vikwazo kama chombo muhimu cha kutoa mashinikizo dhidi ya nchi pinzani

Kwa msingi huo ni wazi kuwa vikwazo vya Marekani vimekuwa na taathira hasi na haribifu dhidi ya mataifa mengine. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaamini kuwa vikwazo vinayarudisha nyuma mataifa kimaendeleo na hivyo kutoa pigo kwa dunia nzima.

Kwa kutilia maanani ukweli huo, kuna udharura wa Umoja wa Mataifa kutoa mashinikizo dhidi ya Marekani kuhusu suala hilo na pia kubuniwa muungano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo hivyo vya upande mmoja, ili kuilazimisha Washington ambayo ni nembo ya kambi ya Magharibi kutazama upya na kubadilisha siasa zake za vikwazo katika uwanja huo.

 

Tags